Na Woinde Shizza,Arusha
Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025 imeendelea na kazi yake kwa kufanya kikao na wananchi wa Mkoa wa Arusha, ikiwa ni sehemu ya mikutano yake ya kusikiliza maoni na ushuhuda kutoka kwa wananchi waliokumbwa au kushuhudia matukio hayo.
Akizungumza wakati wa kikao kilichofanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Arusha, Mwenyekiti wa Tume huru ya uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio ya Oktoba 29, Jaji Othman Chande
alisema Tume hiyo imekuja kufanya uchunguzi juu ya tukio lililotokea tarehe 29 Oktoba 2025, ili kupata ukweli wa chanzo na kujua hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili matukio kama hayo yasitokee tena.
Kwa upande wake, Jaji Paulo Meela, ambaye ni mjumbe wa Tume, alifafanua kuwa Tanzania imeshatumia tume za aina hii mara sita tangu kupata uhuru mwaka 1961.
Alibainisha kuwa tume hizi si za kijinai, bali ni chombo cha kupata ukweli pale kunapotokea tukio kubwa ambalo mamlaka ya juu ya nchi imeona lina hitaji kuchunguzwa kwa kina.
“Wananchi wanapaswa kueleza yale waliyoyaona au kuyashuhudia wenyewe, siyo ya kuambiwa ,lengo ni kupata picha kamili ya ukweli na kutoa mapendekezo ya kitaifa,” alisema Jaji Meela.
Katika kikao hicho, wananchi walipata nafasi ya kutoa maoni na kueleza changamoto mbalimbali zinazohusiana na matukio hayo ambapo mmoja wawananchi aliejitambulisha kwa jina la Swalehe, mmoja wa washiriki, alisisitiza umuhimu wa wananchi wa kila kata kujitokeza kutoa maoni yao mbele ya Tume, akibainisha kuwa ukosefu wa ajira ni chanzo kikuu cha matatizo mengi yanayowakumba vijana.
“Serikali inapaswa kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo na kuhakikisha watumishi wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, Pia sheria na kanuni zisipuuziwe,” alisema Swalehe.
Wananchi wengine, akiwemo Margret Isanja, walieleza masikitiko yao kuhusu matukio yaliyowasababishia hasara na vifo
Naye Samwel Marco Mungure, kijana mwenye umri wa miaka 23, alisisitiza kuwa matukio hayo yanapaswa kuwa “muharubaini wa mabadiliko ya katiba” na kwamba mchakato wa katiba mpya unapaswa kufanyiwa kazi kwa kina.
Kwa upande wake, Bahati Lema alipendekeza vijana washirikishwe zaidi katika tume mbalimbali na kwamba Serikali ianzishe tume maalum ya kushughulikia michezo, kama njia ya kuwajengea vijana matumaini na ajira.
Tume hiyo inaendelea na ziara zake katika mikoa mingine, ikikusanya ushahidi na maoni kutoka kwa wananchi, taasisi na viongozi wa dini, kabla ya kuandaa ripoti yake kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia