KIJAJI ATAKA NGORONGORO ILINDWE ZAIDI, HUDUMA ZA UTALII ZIBORESHWE
Na Woinde Shizza ,Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ametoa maagizo kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Kamishna Abdul Razaq Badru, kuhakikisha hifadhi hiyo inalindwa kikamilifu ili iendelee kuwa na ikolojia yenye mvuto na kuhifadhi rasilimali zake zote za asili.
Dkt. Kijaji alitoa maagizo hayo leo Januari 29, jijini Arusha, wakati wa hafla ya kuvishwa cheo cha Ukamishna wa Uhifadhi kwa Kamishna Badru, sambamba na uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA.
Amesema pamoja na ulinzi wa hifadhi, Serikali inaendelea kuboresha huduma za malazi kwa watalii ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya utalii, hatua itakayoongeza idadi ya vitanda kutoka 1,555 vya sasa hadi zaidi ya 2,590.
Aidha, Waziri Kijaji amemtaka Kamishna wa NCAA kushirikisha wadau mbalimbali katika kubuni na kuibua mazao mapya ya utalii pamoja na kuyatangaza, hususan kupitia taasisi za utalii zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Ameelekeza kuwa kila mwaka angalau kivutio kimoja kipya cha utalii kiingizwe sokoni.
Pia, Dkt. Kijaji amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma za utalii kwa ujumla ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea hifadhi, sambamba na kuimarisha mahusiano kati ya jamii zinazozunguka hifadhi na mamlaka husika, ili wananchi wanufaike zaidi na rasilimali zinazopatikana katika Hifadhi ya Ngorongoro.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia