MKUU WA WILAYA YA ARUSHA AWATAKA WANANCHI KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA WAKATI AKITEMBELEA KAMBI YA MATIBABU YA MOYO




Na Woinde Shizza,Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mheshimiwa Joseph Mkude, ametoa wito kwa wananchi kujiunga na mpango wa bima ya afya ili waweze kupata huduma za matibabu kwa urahisi na gharama nafuu, hususan katika matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo, kisukari, na shinikizo la damu.


Mkude alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika Kambi Maalum ya Matibabu ya Moyo inayoendelea katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwa ushirikiano na Taasis ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ambapo zaidi ya wananchi 800 wamehudumiwa tangu kambi hiyo ianze tarehe 29 Desemba 2025.


Alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa asilimia 32 ya vifo duniani husababishwa na magonjwa ya moyo, hivyo ni muhimu kwa jamii kuchukua hatua mapema kwa kujikinga na kujiunga na mfumo wa bima ya afya.



“Kujinga na bima ya afya kunalinda familia dhidi ya mshtuko wa kifedha pale mwananchi anapougua ghafla magonjwa yanayohitaji matibabu ya muda mrefu au ya kibingwa,” alisema Mkude.


Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya nchini kupitia programu za tiba mkoba ambazo zimewezesha huduma za kibingwa kufikishwa karibu na wananchi.


Mkude pia alishukuru uongozi wa JKCI kwa kuanzisha kambi hiyo katika Mkoa wa Arusha, akisema hatua hiyo imesaidia kupunguza gharama za wananchi kusafiri hadi Dar es Salaam au nje ya nchi kufuata matibabu.


Kwa mujibu wa taarifa za kambi hiyo, hadi sasa zaidi ya wagonjwa 700 watu wazima na watoto 100 wamepatiwa huduma za uchunguzi wa moyo, vipimo vya kitaalamu ikiwemo ECHO na ECG, huku wagonjwa 53 wakifanyiwa tathmini ya upasuaji na 5 kati yao wakifanyiwa upasuaji mkubwa.


Vilevile, wagonjwa 45 wamepewa rufaa kwenda JKCI kwa matibabu zaidi. Kambi hiyo inatarajiwa kuendelea hadi tarehe 9 Januari 2026.


Mkude alihitimisha kwa kuwapongeza wataalamu wote kutoka JKCI na ALMC kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka wananchi wa Arusha na mikoa jirani kutumia fursa hiyo ya uchunguzi na ushauri wa kitaalamu.


“Ushirikiano huu wa JKCI na ALMC ni muhimu sana, hasa tunapoelekea katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, ambapo Arusha itakuwa mwenyeji na masuala ya afya ni sehemu ya maandalizi hayo,” aliongeza.












About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia