ARUSHA YAANDAA TAMASHA KUBWA LA UTALII, UFUNDI, FURSA KWA WAJASIRIAMALI

 



Na Woinde Shizza, Arusha

Jiji la Arusha linatarajiwa kuwa kitovu cha utalii, sanaa, utamaduni na biashara baada ya kuandaliwa kwa Tamasha la Arusha Artisan Festival 2026, litakalowakutanisha mafundi, wabunifu, wawekezaji, wanunuzi na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii.

Tamasha hilo, linaloandaliwa kwa kushirikisha Tanzania International Tourism Festivals (TITF), limepangwa kufanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 11, 2026, katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TITF, Ibrahim Jamal, tamasha hilo linalenga kuunganisha utalii, utamaduni na uchumi wa ubunifu kwa maendeleo endelevu, huku likitoa jukwaa kwa mafundi na wazalishaji wa bidhaa za asili kuonesha kazi zao na kupata masoko mapya.

Jamal amesema kupitia kauli mbiu ya “Your Craft. Your Story Your Market, tamasha hilo litawapa washiriki fursa ya kutangaza kazi zao, kukutana na wanunuzi, kuuza bidhaa na kujenga mahusiano ya kibiashara yatakayosaidia kukuza shughuli zao.

Amesema mbali na maonesho ya bidhaa za ufundi, washiriki watapata fursa ya kujenga mitandao ya kibiashara, kupata masoko mapya, kuendeleza biashara zao na kujifunza kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya utalii na uchumi wa ubunifu.



Kwa mujibu wa Jamal, tamasha hilo linatarajiwa kuwavutia maelfu ya washiriki wakiwemo wajasiriamali, wawekezaji, viongozi wa sekta ya utalii, wabunifu na watunga sera kwa lengo la kujadili na kuibua fursa mpya za biashara na maendeleo.

Aidha, amesema tamasha hilo litakuwa daraja muhimu kwa mafundi wa ndani kupata nafasi ya kukutana moja kwa moja na wanunuzi pamoja na washiriki kutoka maeneo mbalimbali, hatua inayotarajiwa kusaidia bidhaa za Kitanzania kupata masoko makubwa zaidi ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wa ushiriki, kifurushi cha mshiriki wa ndani kinapatikana kwa Sh30,000, huku nafasi ya mwoneshaji wa bidhaa ikigharimu Sh150,000, wakati washiriki wa kimataifa pia wamepewa nafasi ya kushiriki kwa utaratibu maalumu.

Tamasha hilo pia litajikita katika kukuza uwekezaji, biashara, ubunifu, majadiliano ya sera na ushirikiano, sambamba na kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii, utamaduni na bidhaa za ubunifu barani Afrika.

Jamal amewahamasisha mafundi, wajasiriamali na wadau wa utalii kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiandikisha mapema kutokana na nafasi kuwa chache.



Amesema tamasha hilo ni zaidi ya maonesho ya bidhaa, bali ni jukwaa la kuunda, kuunganisha na kustawisha biashara, sanaa na ubunifu.

“One Festival, Countless Opportunities, Endless Impact,”ni ujumbe unaobeba dhamira ya tamasha hilo ambalo linatarajiwa kuacha alama katika kukuza sanaa, ufundi, utalii na uchumi wa ubunifu nchini.






About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia