SUA YAPANUA UWEKEZAJI KIBIASHARA, YALENGA KUJENGA UWEZO WA KUJIENDESHA KWA MAPATO YA NDANI
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha uzalishaji wa mapato ya ndani kwa kuanzisha kampuni ya uwekezaji itakayoratibu na kusimamia vitengo mbalimbali vya uzalishaji visivyo vya kitaaluma, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, tija na uwezo wa Chuo kujiendesha kibiashara.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya SUA katika kipindi cha Awamu ya Sita, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Prof. Raphael Chibunda, amesema SUA kupitia kampuni yake ya uwekezaji ya SUA Income Generation & Services Ltd, inaendelea kutekeleza mikakati madhubuti ya kutumia rasilimali zake katika shughuli zenye uwezo wa kuzalisha mapato na kuchochea maendeleo ya Chuo.
Amesema katika kutekeleza mkakati huo, ukarabati wa majengo ya Kiwanda cha Uchapishaji (Printing Unit) pamoja na Kitengo cha Maziwa (Dairy Unit) umekamilika, huku baadhi ya mitambo ya uchapishaji ikiwa tayari imefungwa na kuwekwa katika hali ya kuanza uzalishaji.
Prof. Chibunda amesema SUA pia inaendelea kutumia mitambo ya Feed Mill & Silos kwa ajili ya uzalishaji wa chakula cha mifugo, kuku na samaki, hatua ambayo pamoja na kusaidia mahitaji ya uzalishaji wa Chuo, inalenga pia kuongeza mapato kupitia shughuli za kibiashara.
Katika kuimarisha uwekezaji wa muda mrefu, amesema SUA imeanza kutumia rasilimali zake za misitu katika fursa za uchumi wa kijani, ambapo Msitu wa Ifinga wenye ukubwa wa hekta 10,000, uliopo Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, unalengwa kutumika katika biashara ya kimataifa ya hewa ukaa (Carbon Trading).
Amesema tayari hekta 1,500 za msitu huo zimepandwa miti ya biashara, hatua inayoweka msingi wa Chuo kushiriki katika soko la kimataifa la hewa ukaa huku kikihakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.
Aidha, amesema SUA imeendelea kuwekeza katika kilimo cha mazao yenye fursa za kibiashara, ambapo katika Shamba la Biashara lililopo Kampasi ya Solomon Mahlangu, jumla ya ekari 200 za mkonge zimepandwa na ekari 100 za mwanzo tayari zimefikia hatua ya kuanza kuvunwa kwa ajili ya uzalishaji wa nyuzi za katani.
Prof. Chibunda amesema katika kuimarisha usimamizi wa shughuli hizo, mwezi Mei 2026 Baraza la Chuo liliunda Bodi ya Usimamizi na kumteua Meneja wa Mpito wa SUA Income Generation & Services Ltd, kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa shughuli za kampuni hiyo.
Amesema kampuni hiyo inatarajiwa kuchukua na kusimamia vitengo vyote vya uzalishaji ambavyo si vya kitaaluma lakini vina uwezo mkubwa wa kuzalisha mapato kwa Chuo, ikiwemo Shamba la Biashara la Kampasi ya Solomon Mahlangu pamoja na vitengo vyake vya maziwa, nguruwe, malisho, shamba na uzalishaji wa chakula cha mifugo.
Vitengo vingine vinavyolengwa kuingia katika uwekezaji huo ni pamoja na Kiwanda cha Samani cha Vuyisile (Vuyisile Mini Furniture Factory) kilichopo Kampasi ya Solomon Mahlangu na SUA Printing Press kilichopo Kampasi ya Edward Moringe.
Kwa upande mwingine, amesema maghala mawili yaliyopo Kampasi ya Solomon Mahlangu yako katika mpango wa ukarabati ili yaweze kutumika kuanzisha kiwanda kidogo cha kuchakata matunda na kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo sharubati, maji ya kunywa pamoja na tomato sauce.
Mbali na shughuli hizo, Prof. Chibunda amesema SUA imeendelea kuwekeza katika maeneo mengine ya kimkakati kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kitaaluma na kuongeza mapato ya ndani, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa chakula cha samaki na mifugo pamoja na uzalishaji wa matofali kwa ajili ya mafunzo na biashara.
Amesema Chuo pia kinaendelea kupanda miti na kununua vifaa vya kisasa vya kukatia magogo katika eneo lake la Msitu wa Mafunzo wa Olmotonyi jijini Arusha, huku kikiboresha Shamba la Mafunzo la Mfano kwa ajili ya kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi, wakulima na wadau wengine.
Kwa mujibu wa Prof. Chibunda, Shamba hilo pia linatumika kama chanzo cha mapato ya ndani kupitia uzalishaji na uuzaji wa miche, matunda, mbogamboga, maziwa, vifaranga vya samaki na bidhaa nyingine za kilimo. Shamba hilo lina mazao na mifugo inayowakilisha kanda mbalimbali za Tanzania, ikiwemo samaki, ng’ombe, mbuzi, kuku, kondoo, ngamia, farasi na sungura.
Aidha, SUA imeendelea kuboresha miundombinu yake katika maeneo mbalimbali, ikiwemo majengo ya Morning Sight kwa ajili ya shughuli za utalii, pamoja na majengo ya Chuo yaliyopo mjini ambayo yanalengwa kutumika katika shughuli mbalimbali za kuongeza mapato.
Katika sekta ya afya, Prof. Chibunda amesema Chuo kimeendelea kuboresha Hospitali ya SUA kwa kuongeza miundombinu ya kutolea huduma, ikiwemo ujenzi wa wodi za wagonjwa na ununuzi wa vifaa tiba, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma bora kwa jamii.
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati mpana wa SUA wa kutumia ipasavyo rasilimali ilizonazo, kuimarisha shughuli za kitaaluma na uzalishaji, kuongeza vyanzo vya mapato na kujenga uwezo wa Chuo kujiendesha kwa ufanisi zaidi kupitia shughuli za kibiashara na uzalishaji wa ndani.
.jpeg)

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia