Mfanyakazi wa kiwanda cha A To Z, Wema salum(18) akiwa amelazwa katika
hospitali ya kituo cha mikutano ya kimataifa cha Arusha( AICC( akidawa
kutelekezwa na majiri wake
KIWANDA cha kutengeneza vyandarua cha A to
Z,kinachomilikiwa na raia wa kigeni mwenye asili ya kiasia, kilichopo kisongo
nje kidogo ya jiji la Arusha, kimelalamikiwa kwa kumtelekeza mfanyakazi wake
baada ya kuugua akiwa kazini na kushindwa kumhudumia.
Mfanyakazi huyo,Wema Salum(18)mkazi
wa Kyela Mkoani Mbeya ametelekezwa katika hospital ya aicc jijini hapa,kutokana
na kuugua maladhi ya malaria kali na homa ya matumbo akifanya kazi kiwandani
hapo na kwamba kabla ya hapo alizidiwa bila kupatiwa msaada wowote wa matibabu
.
Akizungumza na libeneke akiwa wodini
ametundikiwa dripu ya maji katika hospitali ya aicc alikolazwa amesema kuwa,
hakuwahi kumwona kiongozi yoyote wa kiwanda hicho ambaye amefika
walau kumjulia hali kwani hata gharama za matibabu zinazidi kumuumiza kichwa
kwani hajui atazilipaje.
Wema ambaye ni miongoni mwa
wafanyakazi wanaishi katika nyumba za A to Z zilizopo ndani ya kiwandani
hicho,alisema kuwa awali kabla ya kulazwa katika hospitali hiyo alikuwa
akishinda amelala chumbani kwake kwa zaidi ya wiki moja akiwa hoi hajiwezi
kitandani na muda mwingi alikuwa akizimia na kupoteza fahamu .
Aliongeza akiwa
chumbani kwake akijiuguza , uongozi wa kiwanda hicho kupitia kwa matron wake
kiliwahi kumpatia mara moja dawa aina ya Panadol
pekee hadi alipoamua kutoa taarifa kwa ndugu zake ambaye alifika
kiwandani hapo na kumkuta akiwa taabani hajiwezi na
kumchukua kwa kumbeba akisaidiana na watu wengine wanne baada ya
kushindwa kutembea.
‘’siku zote naumwa niliwahi kupatiwa
dawa aina ya panadol tu na uongozi wa kiwanda hicho na hawakuwa tayari
kunipeleka hospital mpaka nilipo pata namba ya shangazi yangu na kumwambia
rafiki yangu ampigie’’alisema wema
Alidai kuwa aliajiliwa na A to Z
mwaka jana yeye na wenzake 33 wakitokea mkoani Mbeya ,kama fundi
wa kutengeneza fulana na kwamba wakati wakiletwa waliahidiwa mambo
mbalimbali kupitia wakala wa kiwanda hicho aliyepo mkoani Mbeya ikiwemo matibabu
,chakula na malazi bure sanjari na malipo manono ya mshahara .
Alieleza kuwa hakuamini kilichotokea
baada ya kuugua,kwani kabla ya hapo aliwahi kuambiwa na wenzake kuwa ukiugua
ugonjwa mkubwa kiwandani hapo kama huna ndugu wa kukusimamia
utajifia.
Alisema licha ya kutoa taarifa kwa
uongozi wa kiwanda hicho ,hakupatiwa matibabu ya aina yoyote zaidi ya kupewa
dawa aina hiyo ya Panadol katika kipindi chote cha wiki moja akiwa chumbani
kwake ,na mara nyingi amedai kila akiulizia matibabu amekuwa akijibiwa na matron
kuwa akizidiwa atajiju.
Naye Eva
Boimanda,ambaye ni ndugu wa Wema aliyekuja kumchukua kiwandani hapo,alieleza
kuwa wakati akimchukua Eva kiwandani hapo,februali 4 mwaka huu
alimkuta katika hali mbaya sana kwani alikuwa hajiwezi kutembea,kula wala
kuongea vizuri na kwamba iwapo angeshinda tena siku hiyo angeweza kupoteza
maisha.
‘’inasikitisha sana yaani mgonjwa ana
muda mrefu na anahali mbaya hakuna anayejigusa hata kumsaidia ,kwakweli huu ni
unyama wa aina gani ,hawa A to Z wanashindwa kumpeleka mtu kutibiwa wanasubili
afe’’alilalamika Eva.
Naye afisa mwajiri wa A
to Z ,Godfrey Obed alisema kiwanda hicho kina utaratibu wa kuwatibu wafanyakazi
wake kupitia hospital ya hindu mandal iliyopo mjini hapa,ila aliongeza kuwa
mfanyakazi huyo alichukuliwa na ndugu zake kibabe na kwenda kumtibu
kusikojulikana.
‘’pindi mfanyakazi anapougua hutoa
taarifa kwa matron na ikibainika ,tatizo ni kubwa taarifa hufikishwa kwa
kiongozi anayehusika ili hatua zaidi za kumpeleka hospital ya
hindu mandal ambako wafanyakazi hutibiwa zichukuliwa’’alisema
Obed.
Aliongeza kuwa Wema wakati akija
kufanyakazi kiwandani hapa alikuwa na kidonda kwenye mguu kilichokuwa kina
msumbua ila kiwanda kilifanyajitihada za kumtibu na kwamba kabla ya kumchukua na
kumpeleka kutibiwa ,ndugu zake walifika na kumchukua.
Hata hivyo alisema kuwa gharama za
matibabu katika hospital anayotibiwa kiwanda hakitahusika kwa kuwa utaratibu wa
kumtibu wagonjwa hutolewa na uongozi wakiwanda hicho na si mtu
yoyote.
Hata hivyo kumekuwepo malalamiko
mengi kutoka kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho wakidai yakuwa wamekuwa hawapatiwi
matibabu kama inavyotakiwa na uwezo wa kiwanda hicho kuwatibu ni kuwapatia dawa
aina ya panadol hata kama unaumwa tumbo ana ugonjwa wowote.
Kiwanda hicho ambacho kiliwahi kutembelewa na aliyekuwa rais wa Marekani,George Bushi,kimekuwa kikilalamikiwa pia kwa kuwalisha wafanyakazi wake chakula cha aina moja ya makande kama dozi,hivyo wengi wao hujikuta wakidhoofu na kukondeana tofauti na kupindi wanakuja kuomba kazi kiwandani hapo.