Habari zilizotufikia hivi punde zinaarifu kuwa Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Shaaban Issa Simba amefariki dunia.
Akidhibitisha kutokea kwa kifo hicho
Shehe Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Sheikh Alhadi Mussa Salim amesema
Mufti amefikwa na umauti hii leo asubuhi katika Hospitali ya TMJ
alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
"Ni kweli Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Shaaban Issa Simba amefariki hii leo asubuhi kwa maradhi ya sukari na presha," alisema kwa ufupi Sheikh Alhhadi.
Mwili
wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo na unataraji
kusafirishwa kesho kwenda mkoani Shinyanga kwaajili ya maziko.
Father
Kidevu Blog inaungana na waislamu wote nchini katika maombolezo na
inawapa pole Familia yake, ndugu jamaa na marafiki na wailsamu wote
ndani na nje ya Tanzania.
INNA LILLAH WA INNA ILLAHI RAJIUN.
Hakika sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu.
SALAMU ZA RAMBI RAMBI
SALAMU za rambi rambi kufuatia msiba huo mzito zimeanza kutoklewa ambapo Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara (Mb.)
ametuma salamu za rambirambi kwa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (BAKWATA) na
Waislamu wote nchini kufuatia kifo cha Sheikh
Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Bin Simba kilichotokea
Jumatatu, tarehe Juni 15,2015 katika hospitali ya TMJ Jijini Dar es Salaam
alipokuwa anatibiwa.
Katika
salamu hizo, Mhe. Mukangara amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kumpoteza
kiongozi huyo ambaye bado Taifa lilikuwa likimuhitaji hasa katika kipindi hiki
cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba
mwaka huu.
Waziri
huyo ameongeza kuwa Mufti atakumbukwa kwa upole
, unyenyekevu wake na kutopenda makuu,wakati wa uhai wake marehemu alikuwa
tayari kumsikiliza kila mtu bila kujali dini au kabila lake.
“Nimepokea
kwa huzuni nyingi taarifa ya kifo cha Sheikh
Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Bin Simba ambaye alikuwa Kiongozi
anayeshirikiana vizuri na viongozi wote wa serikali na vyama mbalimbali katika
kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuwa wamoja” amesema .
Amesema Waziri
Mukangara: “Nakutumia salamu zangu za rambirambi wewe Katibu Mkuu, BAKWATA na
waislamu wote nchini na naungana nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa
katika nchi yetu.
Aidha,
kupitia BAKWATA, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu
kwa kumpoteza mpendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu. Pia,
naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke pema
peponi roho ya marehemu … Amina.”