Makada wanaoomba kupitishwa na CCM kuwania urais
jana walianza kusaka wadhamini kwa staili ya aina yake baada ya Waziri
wa Uchukuzi, Samuel Sitta kuibuka na basi la kifahari atakalotumia
kuzunguka mikoani, huku Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akitua
Mwanza kwa ndege.
Sitta, ambaye alitangaza nia yake ya kuwania urais
juzi, jana alikuwa miongoni mwa makada watatu waliojitokeza kuchukua
fomu za kuwania nafasi hiyo kwenye ofisi za makao makuu ya CCM mjini
Dodoma kabla ya kuanza kusaka wadhamini.
Wengine waliochukua fomu ni Waziri wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Titus Kamani na waziri wa zamani wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo.
Wanaochukua fomu hizo za CCM wanatakiwa kutafuta
wanachama kwenye mikoa 15, huku 10 ikiwa ya Tanzania Bara na mitano ya
Zanzibar na wanatakiwa wapate wadhamini 450 kwa mikoa hiyo na mwisho wa
kurudisha fomu ni Julai 2 wakati vikao vya mwisho kuteua mgombea
vitafanyika Julai 12.
Sitta, ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa,
alianza kutafuta wadhamini mjini Dodoma na alitarajiwa kuendelea na kazi
hiyo kwenye mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe na Mbeya, lakini
kilichovutia zaidi ni basi alilosema amekodi aina ya Yutong ambalo lina
sehemu ya kukaa kama sebule.
Sitta na basi lake
Sitta alifika katika jengo la ofisi hizo za CCM
akiwa ndani ya basi hilo aina ya Yutong, ambalo alisema sehemu yake ya
ndani ilibuniwa na mwanaye.
Ndani ya basi hilo kuna kochi moja kubwa ambalo
linaweza kutumika kama kitanda, kiti cha ofisini na meza ndogo
iliyopambwa na picha yake na maneno “viwango mwaka 2015-2020”.
“Hivi vyote ni vitu vya nyumbani kwangu, kijana
wangu anaitwa Ben alibuni namna (ya kuviweka kwenye basi). Sikutumia
gharama yoyote zaidi ya kukodisha basi,” alisema Sitta akiwa ndani ya
basi hiyo na mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage.
Alisema aliamua kutumia basi hilo la abiria ili
apunguze gharama za utafutaji wa wadhamini katika mikoa 18 anayotaka
kwenda kuwatafuta.
“Unajua nina marafiki zangu kama 11 nataka niwe
nao sasa kutumia usafiri wa magari ni gharama ndio maana tukaamua
kufanya hivi,” alisema Sitta na kuongeza kuwa katika safari zake hizo
atakuwa akisafiri usiku.
Vipaumbele vya Sitta
chanzo;mwananchi
chanzo;mwananchi