Ibrahim Lipumba ni mchumi wa kimataifa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF). Alizaliwa Juni 6, 1952 katika Kijiji cha Ilolangulu mkoani Tabora.
Alipata elimu ya msingi mkoani Tabora mwaka 1959
katika Shule ya Wamisionari wa Sweden waliokuwa Tanzania wakati huo,
shule hiyo iliitwa “Swedish Free Mission Primary School”, alimaliza
mwaka 1962 na akasoma Shule ya Kati (Middle School) mwaka 1962 – 1966
kabla ya kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari
Tabora mwaka 1967 – 1972 kisha akaelekea mkoani Dar es Salaam na kusoma
kidato cha tano na sita katika Shule Sekondari ya Pugu kati ya mwaka
1971-1972.
Alipata shahada mbili za kwanza katika Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) na mbili nyingine amezipata katika Chuo Kikuu
cha Stanford, Marekani ambacho ni miongoni mwa vyuo 10 bora duniani.
Shahada zote nne alizonazo ni za uchumi.
Alisoma na kupata shahada ya kwanza katika uchumi
mwaka 1973 - 1976 na shahada ya Uzamili akiianza mwaka 1976 - 1978.
Lipumba ni miongoni mwa Watanzania waliowahi kuweka rekodi nzito UDSM
katika shahada ya kwanza, ndiye aliyekuwa mwanafunzi bora katika Kitivo
cha Sanaa na Sayansi ya Jamii akiwa amepata daraja la kwanza la juu
kuliko wanafunzi wote (GPA 5) na alitunukiwa zawadi ya Makamu Mkuu wa
Chuo katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii.
Profesa Lipumba alipojiunga Chuo Kikuu cha
Stanford alisoma shahada mbili na kupata ufaulu wa heshima, kwanza
alisoma na kuhitimu Shahada ya Uzamili mwaka 1977/1978 na kisha akasoma
na kuhitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika uchumi kati ya mwaka 1978 –
1983. Kwa ujumla, elimu ya uchumi ya Profesa Lipumba imejikita katika
masuala ya fedha na biashara za kimataifa na eneo la pili ni maendeleo
ya uchumi na uchumi wa kilimo.
Kwa miaka mingi sasa Profesa Lipumba amekuwa
mhimili mkubwa wa masuala mbalimbali ya uchumi duniani, ameshiriki
katika majopo ya wanazuoni nguli wa uchumi duniani katika kutafuta mbinu
bora za kusaidia nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kujikwamua
kiuchumi. Ameshiriki moja kwa moja katika shughuli za kitaalamu
kutathmini uchumi wa nchi nyingi duniani na kutoa mapendekezo ya hatua
za kuchukua, amefundisha katika vyuo vikuu vinavyoheshimika duniani na
amewatumikia Watanzania katika nyanja za kiuchumi kwenye Serikali
kadhaa.
Alianza ajira akiwa mhadhiri msaidizi UDSM na
akawa mhadhiri mwandamizi baada ya kuhitimu PhD, alikuwa profesa
mshiriki kuanzia mwaka 1989 kabla ya kuwa profesa miaka ya 1990.
Kimataifa amekuwa profesa mwalikwa katika Kituo
cha Maendeleo ya Uchumi katika Chuo cha Williams Marekani 1989 – 1993,
mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uchumi
(UNU/WIDER) kilichopo Finland mwaka 1993 – 1995.
Amekuwa akisimamia masuala ya uchumi wa dunia kwa
ngazi ya ushauri wa kimataifa, amekuwa mchumi mshauri wa Umoja wa
Mataifa, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF), UNDP, Sida,
Norad, Danida, mashirika ya kikanda kama Comesa na baadhi ya nchi za
Afrika, Ulaya na Asia.
Amefanya kazi kubwa za kiushauri ili kuinua
mashirika mbalimbali ya umma nchini, amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya
TKAI, NIC, TWICO, Imara Wood Industries, Tume ya Rais ya kushughulikia
masuala ya uchumi wakati wa Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi,
mwenyekiti wa tume kadhaa zilizoundwa na Rais za uchunguzi wa matatizo
ya mashirika mbalimbali ya umma.
Profesa Lipumba amezaliwa na kukulia katika
familia ya kisiasa. Baba yake mzazi ni miongoni mwa waasisi wa Tanu na
alishiriki mkutano wa mwaka 1958 uliojadili kuharakishwa kwa uhuru wa
Tanganyika. Mwenyewe amekuwa kada wa Tanu na baadaye CCM tangu akisoma
hadi alipokuwa anafanya kazi.