January Makamba akitangaza nia ya Urais leo.
Wananchi wakifuatilia hotuba ya Mhe. Makamba katika Ukumbi uliopo Mlimani City, Dar.
Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Mhe. January Makamba leo ametangaza nia ya kuwania Urais
kupitia CCM, ataja vipaumbele vyake vitano vikiwemo Kuinadi ilani ya
CCM, Huduma bora za Jamii, Usimamizi uchumi na Kulinda amani na usalama.
Mhe. January ametangaza nia yake katika Ukumbi uliopo Mlimani City jijini Dar es Salaam jana jioni
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba jana alitangaza nia kwa mara nyingine ya kuwania urais akiahidi serikali yake kuunda baraza la mawaziri wasiozidi 18 wasiotiliwa shaka na wananchi juu ya uwezo na uadilifu wao.
Makamba ambaye alishatangaza nia hiyo mwaka jana
akiwa London, Uingereza alisema ametafakari kwa kina kuhusu changamoto
zinazoikabili nchi na aina mpya ya uongozi inayohitajika na kuamua
kuomba ridhaa ya urais ili azitatue.
Mwanasiasa huyo aliwaambia wananchi waliojitokeza
kumsikiliza kuwa kesho atakwenda Dodoma kuchukua fomu ya kuomba ridhaa
hiyo na kuongeza kuwa; “sijagombea kugombana na watu, nimegombea
kupambana na changamoto za watu. Naiomba nafasi huku nikielewa kiu ya
Watanzania kupata aina mpya ya uongozi wa zama za sasa utakaotoa
matumaini mapya yatakayozaa Tanzania mpya. Naelewa misingi iliyojenga
nchi yetu ya haki, umoja, amani na upendo na mshikamano… inayotakiwa
kulindwa kwa gharama zote.”
Alisema aina ya uongozi wa utakaochaguliwa Oktoba
ndiyo utakaoamua mustakabali wa nchi na majawabu mapya
yatakayomtofautisha yeye na wengine.
Makamba ambaye aliyohutubia kwa takribani saa
1.17, alisema atainadi ilani ya CCM kwa nguvu zote na serikali
atakayounda itaongozwa na falsafa ya uwezeshaji mpana kwa wananchi
kisiasa, kiuchumi na kijamii.
“Sitaunda serikali ya waporaji na wabinafsi.
Nitaunda serikali yenye utu, inayowasikiliza watu, itakayotimiza wajibu
wake bila chembe ya uonevu wala ulegevu… nitaunda serikali ya mawaziri
18 ambayo haitakuwa na mtu hata mmoja anayetiliwa shaka uadilifu wake au
uwezo wake,” alisema Makamba huku akishangiliwa.
Alisema serikali yake itakuja na vipaumbele vitano
vya kukuza vipato vya watu kwa shughuli zote, huduma bora na za uhakika
za kijamii; utawala bora, haki, utawala wa sheria, usimamizi wa uchumi
na kulinda amani, umoja na usalama wa nchi.
Makamba (41) alieleza namna atakavyotekeleza
vipaumbele vyake kama alivyokwisha eleza katika mahojiano yake yaliyomo
katika kitabu cha Padri Privatus Karugendo kiitwacho Maswali na Majibu
40 juu ya Tanzania Mpya.
Kuhusu ukuzaji wa uchumi, mbunge huyo wa Bumbuli
alisema ataunda baraza la uchumi litakalojumuisha wataalamu kutoka
taasisi za umma, magwiji wa uchumi na wawakilishi wa sekta binafsi,
litakalohakikisha uchumi unawekewa mipango ya muda mfupi na mrefu
kutatua changamoto zinazoikabili nchi.
Alisema pia ataziboresha taasisi za kifedha, tume
ya mipango, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
ili kudhibiti matatizo yanayoikabili nchi ukiwamo mfumo wa bei na
kushuka kwa thamani ya shilingi.
Katika mipango yake ya kulinda amani na umoja
alisema ataanzisha jukwaa maalumu litakalojumuisha Baraza za Maaskofu
Tanzania (TEC) Jumuiya Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza Kuu la Waislamu
wa Tanzania (Bakwata) litakalokuwa linakutana na rais kila baada ya
miezi miwili kujadili namna ya kuimarisha umoja, amani na upendo nchini.
Alitaja mambo mengine atakayoyatekeleza kwa
kuyaita majawabu mapya kuwa ni kutatua tatizo la ajira, rushwa,
miundombinu, elimu, maji na umeme.