Na Ahmed Mahmoud
Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA William Mwakilema amesema Maonesho ya Nanenane ni jukwaa sahihi la kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji vinavyopatikana katika Hifadhi za Taifa Tanzania kutokana na watu wengi wa ndani na nje wanaokuja kupata elimu na kununua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wakulima, wafugaji na wafanyabiasha kutoka ndani na nje ya nchi.
Ameyasema hayo katika banda la TANAPA leo tarehe 08.08.2023 alipoungana na watanzania wengine katika maadhimisho ya kilele cha maonesho ya wakulima almaarufu Nanenane yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Akiwa katika banda la TANAPA na baadaye banda la TFS Kamishna Mwakilema alisema, “Taasisi za Maliasili na Utalii zinafurahia uwepo wa maonesho haya ya wakulima kwa sababu ni sehemu sahihi ya kutangaza vivutio vya utalii, kuwatangazia wananchi mazao ya utalii, mazao ya misitu na nyuki, pia kutangaza fursa za uwekezaji unaochagizwa na wingi wa watu wanaohudhuria maonesho haya.”
Aidha, Kamishna Mwakilema aliongeza, “kilimo na mifugo ambayo maonesho haya yanawalenga zaidi, wanategemea maji ambayo vyanzo vyake vikuu vimehifadhiwa katika hifadhi za taifa, vile vile utalii huongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo. Hili linajidhihirisha kwa watalii wanapokuja kutalii nchini wanatumia chakula kinachozalishwa na wakulima na wafugaji wetu.”
Kwa Upande Mwingine Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeendelea kunadi vivutio vya utalii, fursa za uwekezaji na kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi mbalimbali wanaotembellea banda la NCAA katika viwanja vya John Mwakangale Mbeya, Nzuguni - Dodoma na viwanja vya Themi Jijini Arusha.
Afisa Uhifadhi Mkuu kitengo cha Uhusiano wa Umma, Joyce Mgaya amebainisha kuwa katika maonesho hayo muamko wa wananchi kutembelea kwa ajili ya kupata elimu umekuwa mkubwa na wengi wanahamasika kujipanga kwa makundi kutembelea vivutio vya Utalii katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
“Maonesho haya sehemu kubwa ni ya wakulima na wafugaji lakini shughuli hizi zinachangiwa na matokeo ya Uhifadhi endelevu katika maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa ambayo ni vyanzo vya kuleta mvua na vyanzo vya maji yanayotumika kwenye mashamba ya wananchi kwa ajili ya matumizi ya kilimo cha umwagiliaji, ufugaji na maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu.”
Msimamizi wa Banda la NCAA Arusha ambae ni Afisa Utalii Mwandamizi Zaynab Suleiman anabainisha kuwa hamasa ya wananchi kupata elimu ya vivutio imekuwa kubwa na waliowengi wamehamasiska kupanga safari za kutembelea eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hasa kupitia makundi mbalimbali kwa ajili kuwa na safari za pamoja kutokea Arusha.
Kwa upande wake kiongozi banda la nanenane kanda ya Kati Dodoma Afisa Uhifadhi Mkuu Lowaeli Damalu ameeleza kuwa katika juhudi za kufikisha elimu ya uhifadhi na utalii kwa wadau wengi katika maonessho hayo watumishi wa NCAA wanatembelea mabanda yote katika viwanja hivyo ili kuwafikia watu wengi na kuongeza uelewa wa masuala ya uhifadhi na utalii kwa washiriki wa maonesho hayo.
Aidha, msimamizi wa Banda la NCAA katika viwanja vya John Mwakangale Mbeya Afisa Uhifadhi Msaidizi Abdiel Laizer anabainisha kuwa katika viwanja hivyo wananchi wameendelea kupata elimu ya uhifadhi na utalii hususan wa mali kale katika kimondo cha Mbozi na makumbusho ya kimondo cha mbozi yenye vielelezo vya tamaduni mbalimbali na kutaka kujua bei na utaratibu wa kufika katika vivutio hivyo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia