Egidia Vedasto Arusha
Mbunge wa jimbo la Arusha Mrisho Gambo amekabidhi magari mawili ya kubeba wagonjwa (ambulance) kwa kituo cha afya Murriet na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru).
Akifanya makabidhiano katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Stendi ndogo ya Mirongoine, Kata ya Murriet Jijini Arusha, amesema ataendelea kupambania changamoto za wananchi wake, ikiwemo afya na nyinginezo.
Aidha amesema magari hayo yana kiwango kizuri kumhudumia mgonjwa wakati gari linatembea, na kuwataka watumishi wa afya kutowatoza gharama za (Ambulance) Wagonjwa kwani serikali hubeba gharama hizo.
"Nimekuwa nikipata malalamiko kutoka kwa wagonjwa kuhusu kutozwa pesa za kulipia (Ambulance inapotokea dharura, mmemsikia Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa (mount meru) Dkt Kipapi Mlambo, amesema kwamba huduma hiyo ni bure" amefafanua Gambo.
Sambamba na kukabidhi vyombo hivyo pia ameendelea kutatua na kufanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo kwa muda mrefu zimekuwa kikwazo cha maendeleo kwa wananchi hao.
Gambo amewataka wananchi kuiamini serikali kwani inaendelea kutekeleza na kukamilisha miradi mbali mbali kama ilivyoahidiwa, ametaja mradi wa ujenzi wa barabara ya olasiti kwamba mkandarasi anaendelea na kazi, ameahidi kukamilisha ujenzi wa soko la Morombo mapema ili wajasiliamali na wamachinga wafanye shughuli zao katika mazingira rafiki na salama.
Katika mkutano huo aliambatana na viongozi wa taasisi mbalimbali ikiwemo (TALURA) Idara ya maji mkoa wa Arusha (AUWSA), Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Arusha (Mount Meru) na Mhandisi anayesimamia mradi wa TACTICS, viongozi hao wamejibu hoja na maswali waliyoulizwa na wananchi.
"Ninaahdi kuendeleza ushirikiano na Watendaji wa ngazi ya Kata hadi Mtaa ili kuendelea kuibua changamoto na kuzifanyia kazi, msisite kunishirikisha katika kila hatua ili twende sawa" ameongeza Gambo.
Mkazi mmoja wa mtaa wa Fieldforce Kata ya Murriet aliyejitambulisha kwa jina la Irene amelalamikia uwepo wa wakabaji (wezi)wanaofanya uharifu majira ya alfajiri katika mitaa hiyo
"Wamama wanaokwenda sokoni alfajiri na mapema na sisi tunaodamka kuelekea kazini tumekuwa tukikutana na visa vya kupigwa, kuporwa na wengine kukatwa mapanga ambapo hadi sasa ninawajua watu kumi na wawili waliokatwa, tusaidieni kwa sababu watu hawa ni tishio" ameomba Irene.
Naye Diwani wa kata ya Murriet Frances Mbise amemuomba Mbunge kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye kata yake ili wananchi wanufaike na kuharakisha maendeleo yao.
Wananchi wa Kata ya Murriet wakimsikiliza kwa makini Mbunge wa jimbo la Arusha Mrisho Gambo katika mkutano wa hadhara uliofanyikia stendi ndogo ya Mirongoine Jijini humo |
Wananchi katika kata hii wako tayari hata kutoa michango yao kushirikiana na serikali pale inapobidi ili kuweka mazingira yao yao vizuri, na kukamilisha miradi iliyokwama. kwa hiyo nakuomba Mheshimiwa Mbunge utusaidie ili miradi ikamilike kwa wakati, maana wananchi wana imani na serikali hii iliyoko madarakani" ameeleza Mbise
Wananchi kwa kutambua mchango wa Gambo katika utendaji na kutatua changamoto zao wamemzawadi mbuzi na kumvisha mavazi ya kabila ya Kimasai kama ishara ya upendo wao kwake.
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mrisho Gambo(katikati) katika makabidhiano ya magari ya kubeba wagonjwa (ambulance) kwa Watumishi wa kituo cha afya Murriet na Hosptali ya Rufaa MountMeru |