WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa nchini waakisi utashi wa
kisiasa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia na kutekeleza
mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.
“’Utashi
wa kisiasa wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha
mfumo wa utoaji wa Haki Jinai lazima udhihirike kwenu ninyi viongozi
mlio karibu na wananchi. Hata hivyo, utashi huo hauwezi kudhihirika
kwenu iwapo hamtakuwa na nia ya dhati ya kubadilika na kisha kuongoza
mabadiliko kwenye maeneo mnayomwakilisha Mheshimiwa Rais wetu na hususan
katika kuhudumia wananchi,” amesema.
Ametoa
wito huo leo (Jumatatu, Mei 6, 2024) wakati akifungua warsha ya Wakuu
wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya kuwajengea uelewa kuhusu
maboresho kwenye mfumo wa Haki Jinai na utoaji wa haki nchini kwenye
ukumbi wa mikutano wa Tume Huru ya Uchaguzi, uliopo Njedengwa, nje
kidogo ya Jiji la Dodoma.
Amesema
sambamba na suala la utashi, ni lazima viongozi na watendaji wa
Serikali wawe na uelewa wa kutosha ili waweze kuyasimamia na
kuyatekeleza mapendekezo hayo.
Amesema
malalamiko ya wananchi katika masuala kadhaa ndiyo yaliyoweka msukumo
kwa Mheshimiwa Rais kuunda Tume ya Haki Jinai na kuyakubali mapendekezo
yaliyotolewa na Tume hiyo na hatimaye kuigeuza kuwa Kamati ya kuandaa
mikakati utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.
“Hivyo
basi, kwa kuwa ninyi ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais katika maeneo
yenu ya utawala, ni wajibu wenu kuhakikisha kuwa azma ya Mheshimiwa Rais
inatimia kwa kusimamia na kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na
Tume ya Haki Jinai,” amesisitiza.
Akitaja
masuala yaliyolalamikiwa na wananchi, Waziri Mkuu amesema utungaji wa
baadhi ya sheria ndogo katika mamlaka zao ambazo aghalabu hukinzana na
sheria mama. “Mfano ni tozo zinazoanzishwa na halmashauri kama vile
ushuru wa mabango, kodi za maegesho na usimamizi wa matumizi ya maeneo
ya barabara zinasababisha mkanganyiko kwa wananchi kwa kuwajibishwa na
chombo zaidi ya kimoja,” amesema.
Masuala
mengine ni migogoro ya ardhi, matumizi mabaya ya madaraka ya ukamataji
na desturi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuambatana na Wajumbe wa Kamati
za Ulinzi na Usalama katika ziara mbalimbali hata zile zisizohitaji
uwepo wa vyombo hivyo, hali ambayo imekuwa ikisababisha hofu kwa
wananchi na kuwafanya washindwe kufikisha mawazo na kero zao kwa
viongozi hao.
Amewataka
viongozi wote walioshiriki warsha hiyo wazingatie maelezo
yatakayotolewa ili kila mmoja akawe chachu ya mabadiliko ya kifikra,
kimtizamo na kiutendaji katika eneo lake. “Wakuu wa Mikoa na viongozi
wote mlioshiriki katika warsha hii, endeleeni kushirikiana na taasisi za
Haki Jinai katika utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya
kuboresha mfumo na utendaji wa taasisi hizi.”
Amewataka
wazingatie uwepo wa majengo na miundombinu muhimu kwa ajili ya taasisi
za Haki Jinai katika maeneo mapya ya utawala (Wilaya) yaliyoanzishwa.
“Kuna maeneo mengi mapya ya utawala bado huduma za Haki Jinai kama vile
vituo vya Polisi na magereza hazijafika na wananchi wanapata taabu sana
kuzifikia huduma hizo katika Wilaya mama ikiwemo kutembea au kusafiri
kwa muda mrefu,” amesisitiza.
Mapema,
Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange alisema kuwa
ofisi hiyo itasimamia utekelezaji wa maagizo na maelekezo yatakayotolewa
katika warsha hiyo ili dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona
wananchi wanapata haki zao inafikiwa.
“Naomba
nitumie nafasi hii kukuhakikishia kuwa yote ambayo tutajifunza katika
warsha hii na maelekezo yote ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu utatupa
tutahakikisha tunakwenda kuyatekeleza katika mikoa na halmashauri zetu
ili dhamira ya mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai yaweze kufikiwa.”
Naye,
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande
alisema Kamati yao iliundwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Septemba
2023 ili kufanyia kazi ripoti ya Tume iliyokuwa na mapendekezo 333 ya
maboresho ya utendaji kazi wa taasisi za haki jinai katika maeneo
mbalimbali.
Alisema
takwimu zinaonesha kuwa matukio ya uhalifu nchini yanazidi kuongeza
mwaka hadi mwaka na kwamba juhudi kubwa zinaelekezwa kupambana na
uhalifu badala ya kubaini na kuuzuia.
“Moja
ya majukumu tuliyopewa kwenye kamati hii ni kuandaa Mkakati wa Kitaifa
wa Kubaini na Kuzuia Uhalifu unaotarajiwa kuwa nyenzo ya utekelezaji wa
taasisi na mamlaka zote zinazohusika ili kukabiliana na janga la uhalifu
nchini,” alisema na kuongeza kuwa viongozi na watendaji wote watakuwa
na jukumu la kusimamia utekelezaji wa mkakati huo utakaporidhiwa na
Serikali ili malengo yake yaweze kutimia.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia