Na Mwandishi Wetu
Serikali
imetenga kiasi cha TZS bilioni 18.5 kwa ajili ya kuwawezesha
wajasiriamali nchini zitakazotolewa kama mikopo yenye masharti nafuu
kupitia Benki ya NMB.
Makubaliano ya utaratibu wa ufadhili huo
yalitiwa saini leo jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki
hiyo, Bi Ruth Zaipuna, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe kwa
niaba ya Serikali na kushuhudiwa na mkuu wa wizara hiyo, Mhe. Dkt.
Dorothy Gwajima.
Akizungumza kabla ya utiaji saini ya mkataba huo
wa miaka miwili, waziri huyo alisema wafanyabiashara wadogo na wa kati
watakopeshwa fedha hizo kwa riba ya asilimia saba.
“TZS bilioni
18.5 ni hela nyingi za kuanzia lakini kiasi hiki kitaongezeka kwani
lengo la Serikali ni kuifanya mikopo hii kuwa endelevu ili iwafikide
watu wengi,” Dkt Gwajima alibainisha huku akisisitiza umuhimu wa
kuitumia vizuri na kuirejesha kwa wakati.
Aliongeza kuwa fedha
hizo zikiwekezwa vizuri zinaweza kuwa na tija kubwa kimaendeleo kwa
kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha mapato ya kaya.
Dr
Gwajima alisema mikopo hiyo ni sehemu ya utaratibu mpya wa Serikali
kuyawezesha makundi maalum na kuhakikisha wanufaika wake ni wale tu
waliolengwa kupata usaidizi huo.
“Wajasiriamali na
wafanyabiashara wadogo wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kwa
hiyo Serkali kupitia wizara hii ina kila sababu ya kuwakwamua na
kuwawezesha ikiwemo kupitia mikopo hii nafuu ambayo NMB imeanza kuitoa
leo.”
Kwa mujibu wa Dkt Shekalaghe utiaji saini na NMB kukopesha
fedha hizo kumeitimisha mchakato wa wizara yao kuitafuta benki mshirika
katika masuala mbalimbali ya kiutendaji na kimaendeleo.
Akibainisha
kuwa mafungu ya mikopo hiyo nafuu itatoka kila mwaka, katibu mkuu huyo
alisema Serikali imeanzisha utaratibu mpya wa kuyafadhili makundi
maalumu na tayari uandikishaji ya wale wenye sifa stahiki umeanza na kwa
upande wa wajasiriamali pia wanapewa vitambulisho maalum.
Katika
maelezo yake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna alisema
mkataba wa kutoa mikopo hiyo ni kielelezo cha jitihada kubwa
zinazofanywa na benki hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya
Sita kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wote nchini
wakiwemo wale wadogo.
Aidha, alisema benki hiyo ina uzoefu na
uwezo mkubwa wa kuwahudumia wajasiriamali ambao umeifanya kutambulika
kimataifa kama kinara wa kuzifadhili biashara changa, ndogo na za kati
nchini.
“Tuzo tulizozipata mwaka huu katika hilo ni pamoja na
zile za Benki Bora ya Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati na Benki Bora ya
Uwezeshaji wa Biashara Ndogo na za Kati,” Bi Zaipuna alisema.
“Ukweli
huo unadhihirishwa na idadi ya mikopo 129,540 yenye thamani ya TZS
trilioni 2.03 iliyotolewa na NMB kwa wajasiriamali kwa kipindi cha mwaka
2020 hadi 2023,” aliongeza na kueleza kuwa ukopeshaji huo kwa
wajasiriamali wakiwemo wamachinga na boda boda ulikuwa ni wastani wa
mikopo 2,699 kila mwezi na TZS bilioni 42.3 kwa mwezi.
“Historia
ya Benki ya NMB imejengwa kupitia uwezeshaji wa sekta ya biashara ndogo
na za kati, kutoa mikopo na juhudi za kuwafikia wafanyabiashara ni moja
ya vipaumbele katika mpango mkakati wetu,” alifafanua.
Bi Zaipuna
alimwambia Dkt Gwajima kuwa utiaji saini mkataba kati ya NMB na wizara
yake kutapanua wigo wa kuwafikia wafanyabiashara wengi zaidi
wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo nchini.
Pia alisema
taasisi hiyo inajivunia kushirikishwa na Serikali kupitia Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika
utekelezaji wa mipango ya kuwahudumia wajasiriamali kwa lengo la kukuza
biashara zao na kuwapa fursa ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na
pato la taifa kwa ujumla.
Akisisitiza umuhimu wa wajasiriamali
katika maendeleo, Bi Zaipuna alisema shughuli zao ni zaidi ya asilimia
95 ya biashara zote rasmi duniani zikichangia asilimia 50 ya pato la
taifa kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na zaidi ya
asilimia 80 ya ajira zote barani Afrika.
“Pamoja na utoaji mikopo
tunaamini kuwa wafanyabiashara hawa watafaidika pia na huduma nyingine
mbalimbali za kifedha zinazotolewa na benki yetu na hivyo kuwafanya
wakue kibiashara,” alibainisha huku akitilia mkazo umuhimu wa kuwapa
elimu ya fedha ili kuhakikisha wanakuwa na nidhamu nzuri ya matumizi ya
mikopo hiyo.
Monday, May 6, 2024
Serikali kuwakopesha wajasiriamali 18.5bn/- kupitia NMB
Posted by woinde on Monday, May 06, 2024 in Habari MATUKIO | Comments : 0
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia