Na Woinde Shizza, ARUSHA
Chama cha ADA-TADEA kimempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paulo Makonda, kwa kazi nzuri anayofanya katika kutatua matatizo mbalimbali na kukagua miradi ya serikali. ,hatua hiyo imezidi kuwavutia wananchi wengi kujitokeza kwenye mikutano yake, wakiamini wataelezwa wazi matumizi ya kodi zao na jinsi fedha zinazotolewa na Rais zinavyotumika katika miradi iliyokusudiwa na serikali ya awamu ya sita.
Hayo yameelezwa na Katibu Mwenezi Taifa wa Chama cha ADA-TADEA, Zuberi Mwinyi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alibainisha kuwa zoezi hilo la ukaguzi wa miradi ni njia mojawapo ya kuwaweka wazi wananchi kuhusu kodi zao
Mwinyi alisema kuwa zoezi hilo la uwazi na ukweli analofanya Makonda ni zuri, ingawa baadhi ya watendaji ndani ya chama cha Mapinduzi hawalitaki kwa sababu zao binafsi.
Alisisitiza kuwa anachokifanya RC Makonda ni kukisaidia chama katika kuwaaminisha wananchi na wapiga kura kuwa serikali ya chama cha mapinduzi inatatua matatizo yao bila kujali tajiri au masikini, jambo ambalo wananchi wanahitaji katika uwajibikaji wa watendaji.
"Zoezi hili litasaidia sana kuwabana viongozi wasio waadilifu wanaotumia idadi ya watu kufanikisha mambo yao kwa kudanganya hesabu zisizo sahihi katika utoaji wa huduma, Kwa mfano, sehemu inayohitaji kujengwa hospitali wilaya inajengwa zahanati, pesa nyingi zimetolewa na Rais lakini hazimalizi miradi kwa sababu walaji ni wengi na hawajali kwa kuona hakuna wa kuwauliza na kufanya kazi kwa mazoea, hali hii inafanya wananchi wengi kuchukia serikali iliyopo madarakani," alisema Mwinyi.
Mwinyi aliwasisitiza viongozi wa dini kuhakikisha wanawahamasisha waumini wao na kukemea rushwa kwani hata kwenye vitabu vya dini imekatazwa ambapo alisema kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika hili, na wakishamjua Mungu kiroho hata ubadhirifu wa miradi hautakuwepo, kwani kila mtu atajua kuwa kuna siku ataacha mali hizo na atawajibika kwa Mungu kwa dhuluma aliyofanya.
"Mwisho wake unakuwa mbaya kwa baadhi ya viongozi wa serikali wanaoteuliwa lakini hawana uwezo wa kusaidia wananchi Wanasababisha wananchi kuichukia serikali huku wakitumia fedha nyingi za walipa kodi bila msaada wowote ,Wengi wanakuwa na mtandao wao kwa ajili ya kuibia serikali bila kujali kiapo walichokiapa siku ya uteuzi kwa kumtaja Mungu ,Watendaji wakitenda haki, nchi itapata baraka," alisisitiza Mwinyi.
Mwinyi aliongeza kuwa viongozi wa dini wana mamlaka na uwezo mkubwa wa kushawishi waumini wao, hivyo ni vyema wakatumia nafasi zao kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na serikali yake katika kufanikisha zoezi la kukemea ubadhirifu wa fedha za serikali kwani inachelewesha maendeleo ya watu na makazi na kusisitiza kuwa Tanzania imepata bahati ya kuwa na kiongozi mwanamke mwenye maono ya kuifikisha nchi mbali
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia