Wafanyabiashara ndogondogo wa soko la kilombero wamepatiwa elimu ya bima ya biashara lengo ikiwa ni kuwasaidia kurejesha uhai wa shughuli zao pindi wanapokumbwa na majanga ya moto na mafuriko.
Mkuu wa Idara ya Bima kutoka Benki ya NMB, Martini Massawe, (kushoto) akiwa na meneja wa Kanda Baraka Ladislaus wakizungumza na mmoja wa wafanyabiashara wa soko la Kilombero juu ya umuhimu wa bima
Elimu hiyo iliyotolewa na benki ya NMB, kupitia kampeni yake ya ‘Umebima?’ ina lengo la kutoa hamasa na Elimu kuhusu umuhimu wa bima ili kuwawezesha wafanyabiashara wakatie biashara zao bima katika kupunguza machungu wanapokumbwa na majanga.
Akizungumza na wafanyabiashara hao katika soko la Kilombero, Mkuu wa Idara ya Bima kutoka Benki ya NMB, Martini Massawe alisema, lengo la elimu hiyo kwa wafanyabiashara ni kwa ajili ya kutoa suluhu ya majanga ya moto na mafuriko ambayo yamekuwa yakiwakumba na kuwaacha na hasara kubwa.
“Hivi karibuni tumeshuhudia majanga makubwa ya moto na mafuriko yanatokea ndani ya masoko yetu na kuwaacha wafanyabiashara kwenye hasara kubwa baada ya bidhaa zao kuteketea, au kusombwa na maji."alisema na kuendelea;
"Hasara hizo mara nyingi inapotokea wafanyabiashara huanza kuhaha bila kujua pa kuanzia, ndio maana leo benki ya NMB tumekuja kuwapa elimu kuhusiana na bima, faida na namna gani mteja anaweza kuipata itakayomsaidia kurejesha biashara yake” alisema Massawe.
Alisema kuwa Bima wanayohamasisha wafanyabiashara ndogondogo kujiunga ni ile ambayo wanaimudu ya kuanzia sh10,000 kwa mwezi ambayo ni sawa na sh 800 kwa mwezi.
“Bima hii ya sh 10,000 tumeleta kwao maana tunaamini wanaimudu kulipa ambayo ni sawa na sh 800 kwa mwezi na mteja wetu anaweza kufidiwa zaidi ya sh 500,000 hasa kwa janga la moto na mafuriko ambayo tumegundua ndio yanawaathiri zaidi wafanyabiashara katika biadhaa zao sokoni” alisema.
Akizungumzia bima hiyo, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara ndogondogo ndani ya soko la Kilombero, Abdi Mchome alisema kuwa umuhimu wa bima ni mkubwa katika biashara, afya na hata mali tunazomiliki katika kurudisha utimamu wa biashara ilivyokuwa awali.
“Hapa katika soko letu, bidhaa zimeungua zaidi ya mara 10 na tumeona wafanyabiashara wakirejeshewa uhai wa biashara zao kwa wale waliokata bima lakini waliokuwa hawana tumeona jinsi walivyokuwa wanahaha katika taasisi za kifedha kusaka mikopo kurejesha bidhaa zao bila mafanikio kutonana na dhamana kuteketea”amesema Mchome.
Nae mfanyabiashara wa soko hilo, Rehema Lucas, alisema kuwa, wametambua umuhimu wa bima na wameona fursa katika kuikata ili kurejesha tabasamu baada ya machungu ya majanga yanapotokea ambayo wamejikuta wakiangukia kwenye mikopo umiza.
“Mwanzo niliona bima ni muhimu kwa afya na mali zingine kama nyumba na vyombo vya moto, lakini leo nimeona hata mimi mfanyabiashara mdogo ni muhimu kuwa nayo ili kusaidia biashara yangu hata majanga yakitokea kama mafuriko yaliyotukumba Arusha msimu wa mvua iliyopita na kusababisha wenzetu kukimbilia kwenye mikopo ya mitaani”