AGROGHABE YAWAHIMIZA WAKULIMA KUTUMIA MBINU ZA KISASA ZA KILIMO NA UFUGAJI
Na Woinde Shizza ,Mbeya
Meneja Mauzo na Masoko wa kampuni ya Agroghabe, Alex King, amewataka wakulima na wafugaji kote nchini kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo na mifugo ili kuongeza uzalishaji na kupata kipato chenye tija.
Akizungumza jana katika Maonyesho ya Biashara ya Kanda ya Kusini yanayoendelea jijini Mbeya, King alisema changamoto kubwa inayowakumba wakulima na wafugaji ni kutozingatia kanuni za kitaalamu katika shughuli zao.
> “Tunawahimiza wakulima kutumia mbegu zilizoidhinishwa na wizara ya kilimo, kutumia pembejeo sahihi na kufuata kalenda ya kilimo. Kwa upande wa wafugaji, chanjo na lishe bora ni msingi wa kupata mifugo yenye afya na inayozalisha vizuri,” alisema King.
Aliongeza kuwa maonyesho hayo ni jukwaa muhimu la wakulima na wafugaji kupata elimu kuhusu teknolojia mpya, bidhaa bora, na mbinu za kisasa zitakazowawezesha kuongeza kipato.
Mmoja wa wakulima waliohudhuria, Bi. Asha Mwangwa kutoka Kyela, alisema maonyesho hayo yamemsaidia kupata maarifa ya kuongeza uzalishaji wa mpunga na kuzuia magonjwa shambani.
> “Kwa kweli nimejifunza mengi. Sasa najua namna ya kutumia mbolea kwa usahihi na jinsi ya kulinda mazao yangu dhidi ya magonjwa. Nimeamua kuanza mara moja kutumia elimu hii msimu ujao,” alisema Bi. Asha.
King pia aliwataka vijana na wanawake wa mikoa ya kusini kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia kilimo cha kibiashara na ufugaji wa kisasa, akisisitiza kuwa sekta hizo ndizo suluhu ya ajira na kipato endelevu.
Aidha, aliongeza kuwa dawa za mimea zinaboresha afya ya majani, kuongeza uzalishaji, kusaidia kunenepesha matunda, na kuongeza kiwango cha sukari katika miwa, jambo linalosaidia wakulima kupata faida kubwa zaidi.
Maonyesho haya ya biashara ya kanda ya kusini yamekuwa ni fursa muhimu kwa wakulima na wafugaji kujifunza mbinu bora, kupata bidhaa na teknolojia za kisasa, na kukuza kilimo na ufugaji wa kibiashara nchini.



0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia