MIICO YAENDELEA KUELIMISHA JAMII KUHUSU ARDHI NA KUHAMASISHA UJASIRIAMALI


 Na Woinde Shizza , Mbeya 

Shirika la MIICO limeendelea kuimarisha ustawi wa wazalishaji wadogo katika mikoa ya nyanda za juu kusini kwa kuwajengea uwezo katika masuala ya ardhi, ujasiriamali na uendelezaji wa masoko. 

Hatua hii inalenga kuongeza kipato, kupunguza migogoro ya ardhi na kuimarisha usalama wa chakula katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya, Innocent Lupondo, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa MIICO, alisema shirika hilo limekuwa likiendesha mafunzo ya Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya Vijiji ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu usimamizi na utawala wa ardhi.


“Tunawapa wananchi elimu kuhusu wajibu wao, tunawahamasisha washiriki katika mipango ya matumizi bora ya ardhi na tunawasaidia kutetea haki zao pale changamoto zinapojitokeza, tunataka kuona jamii zetu zikisimamia rasilimali zao kwa usahihi na kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Lupondo.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yamekuwa yakihusisha mabaraza ya ardhi ya vijiji, viongozi wa vijiji, vikundi vya wanawake na vijana pamoja na wawakilishi wa jamii.

Alibainisha  Kupitia mijadala ya wazi na mafunzo ya vitendo, jamii imewezeshwa kutatua migogoro ya ardhi na kupanga matumizi bora ya ardhi kwa kuzingatia shughuli za kilimo, ufugaji, hifadhi ya mazingira na maeneo ya makazi.

“Mafunzo haya yameongeza ushiriki wa wanawake na vijana kwenye maamuzi ya umiliki wa ardhi, hili ni jambo la msingi kwa kuwa wanawake na vijana ndio nguvu kazi kubwa ya taifa na wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maisha yao,” alisisitiza Lupondo.

Miradi hii inatekelezwa katika wilaya 13 za mikoa saba ya nyanda za juu kusini, zikiwemo Chunya (Mbeya), Makete, Wanging’ombe na Makambako (Njombe), Rungwe (Mbeya), Nkasi (Rukwa), Mbozi na Momba (Songwe), pamoja na Mpanda, Mlele, Tanganyika na Nsimbo (Katavi).

Mbali na mafunzo ya ardhi, MIICO pia inatekeleza miradi ya ujasiriamali na maendeleo ya masoko kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Green Revolution in Africa (AGRA) kupitia mpango wa Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture (YEFFA),Mpango huu unalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo biashara, kuwawezesha kutumia teknolojia bora na kufungua fursa za masoko.

Kwa mujibu wa takwimu za utekelezaji, hadi kufikia mwaka 2025, jumla ya wanufaika 674 wameshiriki katika programu hizi, wakiwemo watu wazima 417 (wanawake 227 na wanaume 190) na vijana 257 (wanawake 127 na wanaume 130).
“Tunajivunia kuona mabadiliko chanya katika vijiji tunavyofanya kazi,Wananchi sasa wanatambua haki zao za umiliki wa ardhi, wanapanga matumizi bora ya ardhi na vijana wameanza kuwekeza katika kilimo kama biashara, Hii ni hatua kubwa kuelekea ustawi wa jamii zetu,” alihitimisha Lupondo.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

إرسال تعليق

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia