RC MAKALLA AAGIZA MPANGO MKAKATI WA UTALII KWA MAANDALIZI YA AFCON 2027




Na Mwandishi Wetu, Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ameagiza kuandaliwa kwa mpango mkakati wa miaka mitano wa kukuza utalii unaojumuisha maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Akizungumza jana Septemba 25, 2025, katika kikao na wadau wa sekta ya utalii mkoani humo, Makalla alisema mkakati huo utahusisha sekta mtambuka ikiwemo michezo, ili maandalizi ya mapokezi ya wageni na watalii yajikite katika fursa pana za kukuza uchumi wa utalii.

“Mpango kazi huo utahusisha kuwepo kituo cha utalii kitakachokusanya nyaraka, tafiti za wanyamapori na maonesho ya tamaduni za Kitanzania. Timu nitakayoiunda itashirikisha wataalamu wa Serikali na wadau wa utalii ili sote tuzungumze lugha moja kwenye safari ya kukuza utalii Arusha,” alisema Makalla.

Aliongeza kuwa, suala la uhifadhi endelevu, usafi na utunzaji wa mazingira litapewa kipaumbele kwani utalii na uhifadhi ni mambo yanayoshirikiana moja kwa moja.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT),  Neema Yotham Msitha, aliipongeza Arusha kwa kuchukua hatua hiyo na kueleza kuwa Wizara ya Michezo na BMT wako tayari kushirikiana katika utekelezaji wa mpango huo.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Eliufoo Nyambi, alisema wizara imefurahishwa na uamuzi huo wa Mkoa na iko tayari kushirikiana katika maandalizi ya AFCON, huku ikibainisha fursa zinazoweza kuunganishwa na sekta ya utalii.



Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT) Kanda ya Kaskazini,  George Laizer, alisema maandalizi ya AFCON ni fursa ya pekee kwa hoteli za Arusha na Moshi kuongeza uwekezaji katika huduma za malazi na chakula kwa viwango vya kimataifa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Bi. Miriam Kaaya, alisema hifadhi zilizo Kanda ya Kaskazini zina uwezo mkubwa wa kuongeza idadi ya watalii endapo kutakuwa na mikakati ya pamoja ya matangazo na maonesho wakati wa mashindano hayo.



Meneja wa Kituo cha Utalii wa Utamaduni (Cultural Tourism), Bw. Paul Mollel, alisema ni muhimu kuandaa vivutio vya kipekee vya utamaduni vitakavyowaleta wageni karibu na maisha ya Watanzania, jambo litakaloongeza thamani ya safari zao.

Makalla alisisitiza kuwa Arusha kama kitovu cha utalii nchini, lazima iandae mpango wa pamoja unaohusisha wadau wote ili kuhakikisha fursa za AFCON 2027 zinanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

إرسال تعليق

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia