MKUU WA WILAYA AWAHAMASISHA WANANCHI KULINDA MIUNDOMBINU YA UMMA
Na Woinde Shizza Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kuhakikisha miundombinu ya umma inalindwa dhidi ya hujuma na uharibifu, ikiwemo barabara na madaraja yaliyotekelezwa kwa gharama kubwa za fedha za walipa kodi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkude alisema serikali imewekeza mabilioni ya fedha kwenye miradi ya miundombinu kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha miradi hiyo inatunzwa kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mali za umma Tukishirikiana kulinda miundombinu tuliyonayo, tutapiga hatua kubwa katika maendeleo badala ya kutumia fedha nyingi kurekebisha uharibifu unaosababishwa na wachache,” alisema.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alihimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za mapema endapo watabaini mtu yeyote anayehujumu mali za serikali, akisema hatua hiyo itarahisisha kuwakamata wahusika na kudhibiti vitendo hivyo.
Katika kuongeza motisha, Mkude alitangaza kuwa serikali ya wilaya itatoa zawadi ya fedha taslimu kwa wananchi watakaofanikisha kuwabaini wahalifu wanaoharibu miundombinu ya umma, hatua aliyoeleza inalenga kuongeza ari ya uwajibikaji wa kijamii.
Wananchi wa maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha wamepongeza tangazo hilo, wakisema litasaidia kuhamasisha jamii kushirikiana kwa ukaribu zaidi na serikali katika kulinda rasilimali zilizojengwa kwa gharama kubwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walieleza kuwa zawadi hiyo itawafanya wananchi wengi kuwa makini na kuibua taarifa za uharibifu mara moja, jambo litakalopunguza mzigo wa ukarabati kwa serikali.
“Hii hatua itawafanya wananchi wawe walinzi wa kweli wa mali za umma. Kwa mfano, barabara na madaraja yakibaki salama, hata sisi wananchi tutanufaika moja kwa moja katika shughuli za kila siku,” alisema mkazi mmoja wa Murriet.
Ujumbe huo wa Mkuu wa Wilaya umetajwa kuwa chachu ya mshikamano kati ya serikali na wananchi katika kulinda na kuhifadhi miradi ya maendeleo, huku serikali ikiahidi kuendelea kutoa elimu na hamasa zaidi ili jamii iwe mstari wa mbele katika kutunza rasilimali za taifa.




0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia