KARATU: SERIKALI YAHAIDI KUUNGA MKONO SHULE BINAFSI ZA KITAALUMA
Na Woinde Shizza,Karatu
Serikali wilayani Karatu imeahidi kuendelea kushirikiana na shule binafsi zinazofanya vizuri kielimu, ikiwemo Shule ya Tumaini Junior, ambayo imekuwa ikiongoza kwa matokeo bora ya kitaifa na kimkoa.
Ahadi hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dkt. Lameck Karanga, wakati wa mahafali ya 15 ya kuhitimu darasa la saba kwa wanafunzi 78na mahafali ya kuhitimu elimu ya awali kwa wanafunzi 14 kutoka shule ya Tumaini TX.
Akihutubia katika mahafali hayo, Dkt. Karanga alisema serikali itaendeleza ushirikiano na shule zote zinazofanya vizuri ili kuhakikisha watoto wa Karatu wanapata elimu bora na yenye ushindani kitaifa.
“Sisi kama serikali jukumu letu ni kuwaunga mkono wadau wa elimu, hasa sekta binafsi. Tunapaswa kuonyesha mshikamano mkubwa kwao kwa kuwa juhudi hizi zinaongeza heshima kwa taifa. Kama alivyoelekeza Rais wetu Samia Suluhu Hassan kupitia sera ya elimu bure, sisi pia tupo bega kwa bega kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya elimu bora,” alisema Dkt. Karanga.
Aliongeza kuwa wazazi wanapaswa kubadilika na kuhakikisha watoto wanapata elimu badala ya kuwatumia kuchunga mifugo au kuwaoza wakiwa wadogo, hasa katika jamii za kifugaji wilayani humo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shule za Tumaini Junior na Tumaini TX, Modest Bayo, alisema siri ya mafanikio ya shule hiyo ni mshikamano mkubwa uliopo kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.
“Mkakati wetu ni kuhakikisha kila mwaka tunafanya vizuri zaidi kitaifa. Tuna walimu wenye moyo wa kujituma, na hii ndiyo siri ya shule yetu kuendelea kuwa miongoni mwa bora nchini,” alisema Bayo
Naye Mwalimu Mkuu wa Tumaini Junior, Elizabeth Fabian, alisema shule hiyo imefanya mahafali mawili mfululizo mwaka huu ambapo wanafunzi 78 wamehitimu elimu ya msingi na 14 elimu ya awali.
Sherehe hizo zilihitimishwa kwa burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi, huku wazazi na wadau wa elimu wakipongeza mafanikio ya shule hiyo na kuahidi kushirikiana kwa karibu zaidi katika kuinua kiwango cha elimu wilayani Karatu.





0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia