Na Woinde Shizza ,ARUSHA.
Benki ya
Posta ( TPB) imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 200 kwa Wanajeshi
Wastaafu wa Jeshi la JWTZ nchini ili waweze kujiendeleza kiuchumi na kuboresha
maisha yao baada ya kustaafu .
Mkurugenzi
wa Mikopo wa Benki hiyo Henry Jonathan amesema kuwa wametoa mikopo hiyo kwa
kipindi cha miaka mitatu tangu waanze kutoa mikopo kwani benki hiyo inaongoza
kwa kutoa mikopo mingi kwa wastaafu ambayo inawasaidia kuinua hali ya maisha na
kuanzisha miradi ya uzalishaji.
Kwa Mkoa wa Arusha wenye jumla ya wastaafu 600
wametoa bilioni 13.7 za mikopo kwa
wastaafu hao ambao ni wanufaika wakubwa wa fursa hiyo ya mikopo.
“Kama
unavyojua benki ya posta inaongoza kwa kutoa mikopo kwa wastaafu ili kuboresha
maisha yao na kuhamasisha uwekezaji wenye tija utakaoinua vipato vyao na jamii
kwa ujumla” Alisema Mkurugenzi huyo
Mwenyekiti
wa Umoja wa Wanajeshi wastaafu unaofahamika kama MUWATA, Luteni Mstaafu Geofrey Wapalila amesema kuwa mikopo hiyo imewasaidia
kufungua biashara na kuwa wajasiriamali hasa wanapoanza maisha uraiani hivyo
kuendeleza maisha yao vizuri pia wameishukuru benki hiyo kwa kuwaamini.
Pia ameiomba
benki hiyo kutoa mikopo ya vifaa kwa wajasiriamali ili waweze kuzalisha kwani
bado wana nguvu za kufanya shughuli za uzalishaji.
Mmoja wa
Wastaafu hao Leonard Kilasi ameshauri
wastaafu hao kukopa kwa busara na kulipa kwa wakati ili mikopo hiyo iwe na tija
na kusaidia maisha yao.