Ticker

6/recent/ticker-posts

WAFANYABIASHARA TANZANITE WAOMBA KONGAMANO.

WAFANYABIASHARA wa madini mkoani Arusha, wameiomba Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) iandae Jukwaa la Fursa la Kibiashara la tanzanite, kuzungumzia changamoto zinazowakabili.
Wamesema sekta ya madini ni moja ya sekta kubwa nchini, inayoinua uchumi wa nchi. Lakini, walisema sekta hiyo ina changamoto kubwa zinazopaswa kutatuliwa.
Mmoja wa wafanyabiashara wa madini ya tanzanite, Japhet Shoo, alisifu jitihada za jukwaa hilo.
Alisema ni lazima serikali ijiulize ni kwa nini bado mpaka sasa haijanufaika na madini ya tanzanite.
Amesema jambo kubwa linalowasumbua wamiliki na wachimbaji wa madini ni upatikanaji wa zana za uchimbaji, kwani shughuli hiyo inapaswa kufanywa na wafanyabiashara wengi na kwa bei poa. Aliomba serikali kuondoa kodi ya uingizaji wa zana za uchimbaji.
Changamoto nyingine inayowakabili wamiliki wa migodi ni zana za uchimbaji, kwa kuwa zinauzwa na watu wachache.
Naye Julius Laizer anayechimba madini ya tanzanite, amesema uongozi wa juu wa TSN unapaswa kupongezwa kwa kuwa wabunifu na kuwahamasisha wafanyabiashara, kueleza kero zao kupitia magazeti yao na kisha kuyafanyia kazi kwa kuwauliza watendaji wa serikali na kupata majibu sahihi ya kero hizo.
Laizer alisema watendaji wa serikali, wamezidiwa na majukumu ya kila siku, hivyo wamesaidiwa kwa namna moja ama nyingine na Jukwaa la Fursa ya Biashara, linaloandaliwa na kampuni hiyo ili kila mfanyabiashara afanye kazi kwa uwazi na uhuru bila ya kuwa na migongano.
Alisema wachimbaji na wauzaji wa madini nchini, wana changamoto nyingi, ambazo zinatakiwa kupatiwa majibu sahihi ili sekta hiyo iweze kuendelea kwa faida ya uchumi wa nchi yetu.
Mfanyabiashara huyo alisema mahali pekee panapotakiwa wao kutoa dukuduku zao ni Jukwaa la Biashara la TSN.
Alisema angependa siku hiyo Waziri wa Madini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini na Kamishna wa Madini wawepo ili changamoto zao ziweze kupata majibu.
Mfanyabiashara mwingine, Hassan Juma, muuzaji na mnunuzi wa madini alisema wafanyabiashara wa madini mkoani Arusha, hawakualikwa katika jukwaa hilo.
Aliusifu uongozi wa TSN kwa kubuni mbinu ya kukutana na wafanyabishara na kueleza kero zao na kuzianika katika magazeti ya serikali na kwa muda mfupi zinapatiwa majibu sahihi na kwa wakati.
Juma alisema kuwa kipindi kijacho, jukwaa hilo linapaswa kutoa kipaumbele kwa sekta ya madini, kwa kuwakutanisha wafanyabiashara wote wa mkoa wa Arusha na wamiliki wa migodi, ili kila mmoja aweze kusema matatizo yanayomkabili.

Post a Comment

0 Comments