Ticker

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI YA MERU YAONGOZA UMITASHUMTA MKOA WA ARUSHA


Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl.Sara Kibwana amesema Halmashauri ya Wilaya ya Meru imeibuka mshindi wa kwanza na wa  jumla ngazi ya Mkoa kwenye mashindano  ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) yaliyofanyika tarehe 06 Juni 2018 hadi 10 Juni 2018 ambapo Halmashauri 7 za Mkoa wa Arusha zilishiriki .

Aidha alifafanua kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru imezawadiwa vikombe 5 kutokana na kuwa mshindi wa kwanza kwenye mpira wa miguu wavulana, Mpira wa wavu wasichana, Mpira wa mikono wasichana na Mpira wa kengele  pia ilikuwa mshindi wa pili kwenye mchezo wa mpira wa wavu wavulana.
 
Kibwana alisema siri ya ushindi huo ni pamoja na maandalizi mazuri yaliyofanyika kwani Halmashauri hiyo ilitoa maelekezo  zaidi ya miezi 9 iliyopita kwa Walimu Wakuu  wa Shule za Msingi kuhakikisha kila wiki wanafunzi wanakua nasiku za kufanya  michezo pia maandalizi yalikuwa mazuri wakati wa michezo kwakuwa wachezaji walijiandaa kikamilifu kwa kukaa siku 5 kambini.

 Naye Afisa utamaduni wa Halmashauri  ya Wilaya ya Meru, Senyaeli  Pallangyo alisema uchaguzi wa wachezaji kwa kuzingatia viwango uliofanyika kuanzia ngazi ya chini hadi Wilaya umechangia  ushindi huo mkubwa ikiwa ni pamoja na uwezo wa makocha sambamba na wachezaji  kuwa na nidhamu ya hali ya juu  na kufuata taratibu za michezo .

Jumla ya wachezaji 25 kutoka timu mbalimbali za Halmashauri yaWilaya ya Meru na Makocha 4  wamechaguliwa kuunda timu ya Mkoa wa Arusha .

Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Meru kwa mwaka huu 2018 imekuwa mshindi wa kwanza  na wajumla kwa ngazi ya Mkoa wa Arusha wenye Halmashauri 7 katika mashindano ya michezo ya umoja wa michezo Shule za Sekondari Tanzania ( UMISSETA) na  umoja wa michezo na taaluma shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na kuzawadiwa jumla ya Makombe ya ushindi 10

Post a Comment

0 Comments