Ticker

6/recent/ticker-posts

KISIMIRI YASHIKA NAFASI YAPILI KITAIFA KATIKA MATOKEO YA KIDATO CHA SITA 2018 .




Na Woinde Shizza,Arusha 

Shule ya Sekondari Kisimiri iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru ,Mkoani Arusha  imefanya vizuri kwenye matokeo ya kidato cha sita  kwa kushika nafasi ya  pili kitaifa kati ya shule 543 zilizofanya mtihani huo, huku shule ya Sekondari Kibaha ikishika nafasi ya kwanza na shule ya Sekondari Kemebos ikishika nafasi ya tatu,hii ni kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na baraza la mitihani Taifa.
Aidha matokeo haya ya shule ya Sekondari Kisimiri ni mwendelezo wa historia ya kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani hiyo ya kidato cha sita kwani kwa miaka 3 mfululizo imekuwa kwenye kundi la shule tatu bora kitaifa ,ambapo mwaka 2016 ilishika nafasi ya kwanza,mwaka 2017 ikashika nafasi ya tatu na kwa mwaka huu 2018 imeshika nafasi ya pili kitaifa kwa watahiniwa wake 67 kupata daraja la kwanza na la pili ikiwa 51 kati yao wamepata daraja la kwanza na 16 kupata daraja la pili.
Nuru ya shule hii ya Sekondari Kisimiri yazidi kuangaza kwenye Mkoa wa Arusha wenye shule 31 zenye watahiniwa zaidi ya 30 za Serikali na Binafsi kwani ni shule pekee ya Serikali kushika nafasi ya kwanza mkoani hapa kwa kipindi cha miaka 3 mfululizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Ndg. Christopher Kazeri alipokuwa akiwapongeza walimu wa Shule ya Sekondari Kisimiri kwa jitihada zao zilizo ifanya shule hiyo kuwa mshindi wa pili kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka huu 2018, pia amewasihi walimu hao kuongeza bidii katika ufundishaji ili kupata matokeo mazuri zaidi kwa kushika nafasi ya kwanza Kitaifa.
Mkurugenzi huyo ametoa pongezi hizo alipotembelea Shule hiyo kwa Lengo la Kuwapongeza Walimu pamoja na kusikiliza na kutatuo changamoto wanazokabiliana nazo ili kuleta tija zaidi kwenye taaluma ya Shule hiyo.
Makamu mkuu wa shule ya Sekondari Kisimiri Mwl. John Awe amesema kuwa mojawapo ya mbinu zilizotumika kuhakikisha shule hiyo inapata matokeo mazuri illikuwa kutoa mafunzo ya ziada kwa wanafunzi ambao walikuwa na uwezo mdogo, hivyo walimu walitenga muda wa ziada kuwafundisha wanafunzi hao ambao wengi wao walifanya vibaya kwenye mtihani wa utamirifu (MOCK) kwa kupata alama sifuri.Ameongeza pia walimu wana moyo wa kufundisha kwa kutoa mfano kuwa kwenda darasani ni swala moja na kufundisha kama inavyotakiwa na wanafunzi kuelewa ni jambo jingine .
Nao Walimu wametoa changamoto zinazoikabili Shule hiyo ni upungufu wa viti vya walimu 50 pamoja na madawati ya wanafunzi 300 pia walimu hao wamehitaji ufafanuzi wa maslai yao kama watumishi ikiwemo kupanda daraja,
Akitoa ufafanuzi wa maswala ya watumishi Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu .Grace Mbilinyi ameeleza kuwa kutokana na zoezi la kuwabaini watumishi hewa na wenye vyeti vya kugushi Serikali ilisitasha upandaji madara kwa watumishi wa umma ila kwa sasa maelekezo mbalimbali yanatolewa ambapo zoezi hilo linaendelea kwa awamu pia
Kuhusu swala la malipo ya likizo amewasihi walimu kuwa makini kwa kuweka viambatanisho vyote muhimu vikiwemo vyeti vya watoto vya kuzaliwa na vyeti vya ndoa pia ametoa angalizo la udanganyifu kwa kugushi vyeti hivyo.

Post a Comment

0 Comments