Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan mapema leo akiwa katika
picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Songwe
(walioko mstari wa nyuma) kabla hajaondoka kuelekea Mkoa wa Mbeya.
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara ya
siku tano Mkoani Songwe mapema leo na kusisitiza ushirikiano baina ya uongozi
ili kuharakisha maendeleo.
Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema akiwa ziarani katika wilaya za Momba, Mbozi na Ileje amebaini
kuwa Mkoa wa Songwe umebarikiwa kuwa na rasilimali na utajiri mkubwa kinachotakiwa
ni viongozi kushirikiana katika kuwatumikia wananchi.
“Nimefurahishwa na
kaulimbiu yenu ya maendeleo yataletwa na sisi wenyewe kwa ushindani na
ushirikiano, bila ushirikiano hakuna maendeleo, kauli mbiu hii sasa ionekane
kwa vitendo”, amesisitiza.
Ameongeza kwa
kuwataka watendaji na viongozi wote wapende kuwatembelea wananchi kuanzia ngazi
za vijiji ili waweze kuwahudumia vizuri na sio kukaa ofisini.
Mhe Samia Suluhu
Hassan ameongeza kwa kuzitaka halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya
kuwakopesha wanawake na vijana na kubuni miradi mikubwa itayaowaunganisha wajasiriamali
wanawake na vijana kutengeneza viwanda ili kuondokana na umasikini.
Amesema mpango wa
mkoa wa kuanzisha vituo vya maendeleo vya kata utawezekana na kuwanufaisha
wananchi endapo watendapo watajitoa kwa dhati kuufanikisha na mpango huu
utaiwezesha Songwe kupaa kiuchumi.
Aidha Mhe Samia
Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Mkoa wa Songwe kuendelea kutunza mazingira
kwa kupanda miti na wale walioko mipakani kuendelea kutunza amani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Chiku Gallawa ameshukuru Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kufanya ziara
mkoani Songwe kuahidi kuwa maelekezo na maagizo aliyoyatoa atayasimamia
yatekelezwe.