Na Woinde Shizza,Arusha
wafanya biashara wa soko la Tengeru lililopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru
wameunga mkono zoezi la kuwaondoa wafanya biashara wa mazao
barabarani kwa kuwaingiza katika eneo la soko.
Afisa biashara ambaye ni msimamizi wa masoko Elibariki Nnko ameeleza
kuwa zoezi hilo limeanza rasmi baada ya baadhi ya wafanya biashara
kukaidi kutumia eneo la soko lililojengwa kwa gharama kubwa na
kuendelea kupanga bidhaa zao barabarani ikiwa ni kuatarisha maisha yao.
Aidha alifafanua kuwa Halmashauri hiyo inaendelea na uboreshaji wa
miundombinu kwenye soko hilo kwani mpaka sasa kiasi cha sh. milioni
20 zimetengwa kwa ajili ya kutengeneza meza za sokoni hapo .
Elisifa Boniface ambaye ni mfanyabiashara kwenye soko hilo alisema kuwa
wateja wengi hawaingii ndani ya soko kwani hupata mahitaji yao nje ya
soko jambo linalo athiri biashara yake na wafanya biashara wenzake
waliopo ndani ya soko.
kwa upande wake Mary Pallangyo ambaye ni mfanya biashara wa mbogamboga ameiomba
Halmashauri hiyo kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na kukamilisha
uwekaji paa kwenye baadhi ya maeneo ya soko hilo.
pia kuna baadhi ya wafanya biashara walio kuwa wakipanga bidhaa zao
barabarani wameiomba Serikali kuwaruhusu kuendelea kujitafutia risiki
kwa njia hiyo.