Ikiwa ni siku 11 tu
kupita toka Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha (SACP) Ramadhani Ng’anzi kuahidi
kurudisha utulivu katika tarafa ya Manyara wilayani Monduli, kwa sasa eneo hilo limezidi kuimarika
kiusalama baada ya kufanyika doria na operesheni za mara kwa mara na jana katika
mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Barafu Mto wa Mbu alizindua vikundi
Tisa vya ulinzi shirikishi vilivyokuwa na jumla ya askari 215.
Awali Kamanda
Ng’anzi aliitoa ahadi hiyo alipokutana na viongozi wa Kata, Vijiji na Vitongoji
katika kikao kilichofanyika ofisi ya Afisa tarafa tarehe 19 Julai mwaka huu
ambapo viongozi hao walisema suala linalosababisha kuwepo kwa matukio ya
uhalifu ni uhusiano hafifu baina ya baadhi ya askari Polisi, viongozi na
wananchi hali ambayo inatoa mwanya kwa wahalifu kuendelea kufanya uhalifu.
Baada ya kuwasikiliza
kwa umakini alibaini baadhi ya mambo ambayo yanayotakiwa yafanyike kwa haraka
ikiwa ni pamoja na kufanya doria na operesheni usiku na mchana, askari Polisi
kutoa huduma bora kwa wananchi hali ambayo itasaidia kuwa karibu nao na kupata
taarifa za uhalifu lakini pia uanzishaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi
katika kila kitongoji ambapo aliwahakikishia viongozi hao kwa kusema kwamba eneo
hilo litakuwa salama.
Kufuatia mikakati
hiyo ya Kamanda Nga’nzi ambaye alisema yeye anapenda sana kutenda badala ya
maneno mengi, siku hiyo hiyo aliongeza askari katika eneo hilo ambao walifanya
operesheni katika maeneo tete, kwenye bar na nyumba za kulala wageni lakini pia
alipiga marufuku kwa waendesha boda boda na Bajaji kufanya biashara hizo mpaka
asubuhi.
Nao viongozi wa eneo
hilo hawakuwa nyuma na kuamua kumuunga mkono kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi
shirikishi kama jinsi alivyoagiza, ambavyo vilipewa mafunzo toka kwa Maofisa
toka Kitengo Polisi Jamii mkoa lakini pia kuahidi kutenga eneo na kujenga kituo
kikubwa cha Polisi.
Katika mkutano huo
uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wakazi wa eneo hilo, aliwasitizia wananchi watoe
ushirikiano wa kutosha kwa askari hao kwa kuwafichua wahalifu ili taarifa zao
zifanyiwe kazi.
Kamanda Ng’anzi
alikiri kuwepo kwa upungufu wa askari Polisi na kusema kwamba uwepo wa vikundi
hivyo vya Ulinzi Shirikishi utasaidia kupunguza pengo hilo huku akisisitiza
uwepo wa amani utasaidia kukuza uchumi kwa wafanyabiashara wa eneo hilo ambao
mara nyingi wanawahudumia watalii wanaokwenda na kurudi toka katika vivutio
mbalimbali.
Kwa upande wake
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo cha JKT Makuyuni Luteni Kanali Phesto Mbanga
aliahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuimarisha ulinzi eneo hilo la
tarafa ya Manyara na kuwasisitiza wananchi nao wasibaki nyuma kwani suala la
amani ni wajibu wa watu wote.
Awali akitoa taarifa
juu ya mafunzo hayo kabla ya kumkaribisha Kamanda wa Polisi, Mkuu wa Kitengo
cha Polisi Jamii mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Edith Makweli
alisema kwamba askari hao walifundishwa namna ya ukamataji salama,upekuzi, haki
zao wanapokuwa kazini, silaha wanazotakiwa kutumia wakiwa kazini na Utii wa
sheria bila shuruti.
Alisema mbali na mafunzo
kwa askari hao lakini pia kwa kipindi cha wiki moja waliweza kutoa elimu kwa
viongozi wa kata, vijiji na vitongoji juu ya wajibu wao, wamiliki wa nyumba za
kulala wageni, Bar na Hoteli ambao wanatakiwa kuwa na leseni halali na
kuhakikisha kwamba kumbi zao zipo salama. Aidha kwa upande wa madereva wa
Bajaji na Boda boda walifundishwa mbinu za kupambana na uhalifu ikiwa ni pamoja
na namna ya kutoa taarifa pamoja na sheria za usalama barabarani.
Baadhi ya wananchi wa tarafa ya Manyara wilayani Monduli wakimsikiliza Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha (SACP) Ramadhani Ng'anzi wakati alipokuwa anaelezea mikakati iliyowekwa na Jeshi la Polisi ya kuzuia uhalifu katika eneo hilo.(Na Woinde Shizza,Arusha )
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi akiongea na wananchi wa Mto wa Mbu
wilayani Monduli wakati wa mkutano wa uzinduzi wa vikundi Tisa vya
ulinzi shirikishi vilivyokuwa na jumla ya askari 215.
Kamanda wa Polisi mkoa wa
Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi
pamoja na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo Cha JKT Makuyuni Luteni Kanali
Phesto Mbanga wakiungana na wahitimu wa mafunzo ya Ulinzi Shirikishi
kimba nyimbo za hamasa baada ya uzinduzi wa vikundi hivyo..