Ticker

6/recent/ticker-posts

Hamasa Ya Wananchi Kuhamia Msomera Ni Ishara Njema Katika Kuihifadhi Ngorongoro - Msemaji Mkuu Wa Serikali .

 


Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Bw. Gerson Msigwa ameeleza kuwa hamasa na idadi kubwa ya wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni ishara njema ya kuokoa uhifadhi na uimarishaji wa shughuli za utalii katika hifadhi hiyo.

Msigwa ametoa maelezo hayo leo tarehe 15 Septemba, 2022 wakati wa kuaga kundi la 9 la wananchi kutoka eneo la Ngorongoro wanaohamia Msomera Handeni Mkoani Tanga.

Amebainisha kuwa kwa sasa Wananchi wengi wameshaelewa umuhimu wa kuiacha hifadhi na kujiandikisha kwa wingi na sasa serikali inaangalia namna ya kuongeza huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo wanayohamia ili kupeleka idadi kubwa zaidi ya wananchi walioko tayari.

“Hamasa hii ni ishara ya jitihada za kuhifadhi Ngorongoro isipotee na wananchi hawa wameona kuendelea kubaki ndani ya Hifadhi wanakosa huduma za msingi ambazo wananchi wa maeneo mengine wanazipata na naamini hata waliokuwa wanapinga zoezi hili wameelewa.” Ameeleza Msigwa.

Ameongeza “Sasa hivi elimu kwa wananchi ipo ya kutosha na uandikishaji ni mkubwa, kwa upande wetu Serikali kwa sasa tunaangalia namna gani ya kuongeza kasi ya miundombinu ili kuhamishia wananchi wengi zaidi ambao wameshajiandikisha na wako tayari kuondoka na kupisha hifadhi”

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Raymond Mangwala amebainisha kuwa tangu wiki iliyopita Serikali ilipoboresha zoezi la uandikishaji wa wananchi kwa kuwatumia watendaji wa vijiji kwenye maeneo yao badala ya timu moja kuzunguka Tarafa nzima imerahisisha wananchi kujiandikisha kwa wingi na zoezi linaenda kwa usalama, amani na uzingatiaji wa haki za binadamu.

Akitoa taarifa ya zoezi hilo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Dkt. Christopher Timbuka amebainisha kuwa hadi kufikia tarehe 15 Septemba 2022 jumla ya makundi 9 yameshahama katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kufanya jumla ya kaya 223 zenye watu 1,233 na Mifugo 7,442 kuhama hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera.

Diwani wa Viti Maalum kata ya Eyasi Veronica Mertuda, ameishukuru Serikali kwa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi na wao kufikia uamuzi wa wananchi wengine waliokwishahamia kwenda maeneo yenye uhuru wa kufanya shughuli za kibinadamu, huduma bora za kijamii na kuwaachia Wanyamapori uhuru kwenye maeneo yao ya asili.

Mzee wa kimila Laigwanani Naftali Mollel kutoka kata ya Endulen ameongeza kuwa “Tumehamasika na kuamua kujiandikisha kwa wingi ili tuipishe hifadhi iendelee kutuingizia mapato, wanyama wamekuwa wengi na watalii wamekuwa wengi, tunaomba wote ambao wanatamani kuondoka wafanye maamuzi, wakati ni sasa na Serikali ya awamu ya sita ipo tayari kuwasaidia” ameongeza mzee Mollel.

Post a Comment

0 Comments