Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI- UKATILI WA KIJINSIA BADO UPO JUU

 

Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii Jinsia na Makundi Maalum Dk. Nandera Mhando akifungua kongamano la tisa la Aquarium kutoa matokeo ya utafiti lilioandaliwa na Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) na Hospital ya Taifa Muhimbili.

SERIKALI kupitia kwa Wizara ya Maendeleo Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum imesema kuwa ukatili wa jinsia na watoto kwa ujumla uko juu kwa asilimia 76 kwa wanawake ukilinganisha na wanaume.

Hayo yameelezwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka wizara hiyo, Dk Nandera Mhando wakati wa kongamano la tisa la ushiriki wa tafiti na sekta katika kukabiliana na changamoto ya ukatili na afya ya akili.

Dk. Mhando amesema ukatili wa watoto uko juu, kutokana na mabadiliko ya tabia, kukua kwa miji, mahusiano na kuelimika kwa vyombo vya habari katika kuongeza kuripoti matukio mbalimbali ya ukatili.

Amesema maeneo yanayoongoza kwa ukatili wa kijinsia ni Kanda ya Ziwa na ukatili kwa watoto mikoa inayoongoza ni Manyara, Arusha, Dar es Salaam na kwamba ukatili unaoongoza ni ubakaji, kipigo, kunyanyaswa kisaikolojia na ukatili kingono.

Dk. Mhando amesema: "Katika kongamano hili tumeona afya ya akili imesababisha ukatili kwa sababu hakuna tafiti ya nchi nzima inayotoa takwimu halisi, huu uwe mwanzo wa kufikisha habari na chachu ya kufanya tafiti nyingine zaidi ili kupata uhalisia kitaifa."

Amesema sababu kubwa zinazochangia ukatili wa kijinsia ni wivu wa mapenzi kwa wanandoa, watoto kuoneshwa vitu vilivyo nje ya uwezo wao hivyo kuwafanyia ukatili watoto wenzao, afya ya akili kwa kuwa na msongo wa mawazo na kushindwa kuhimili changamoto zinazowakabili.

"Wazazi na walezi kuwa karibu na watoto, wanapofanya makosa haya hatuwezi kusema kama wamenuia kwa sababu anajifunza vitu chini ya umri ao hivyo wanapoendelea kujaribu inakuwa mazoea wanajaribu kufanya kile walichokiona hivyo kukinzana na sheria," alisema Dk. Mhando.

Pia Dk. Mhando amefafanua kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo uwepo wa nyumba salama 10, vituo vya mkono kwa mkono 21 vinavyotoa huduma jumuishi katika hospitali, vituo vya kupokea watoto waliotelekezwa na kuwahudumia pamoja na kuwaunganisha na wazazi wao.

Kwa upande wake Mhadhiri na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas), Dk Jessie Mbwambo alisema kati ya watu 100 waliohojiwa, 15 walieleza kuwa walipata mawazo ya kujiua kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Dk. Mbwambo amesema kati ya mwaka 2019 na 2020 wanawake 44 sawa na asilimia 72 walikufa kutokana na wivu wa mapenzi.

Ameeleza kuwa watoto saba kati ya wanafanyiwa ukatili kwa kupigwa wawapo shuleni na nyumbani huku watoto watatu kati ya 10 wamefanyiwa ukatili wa kingono kwa kubakwa kabla ya miaka 18.

"Julai mwaka 2021 watuhumiwa 275 walikamatwa kwa makosa ya mauaji na kati yao 21 wanadaiwa kuwaua wapenzi wao. Tumeona mila potofu zinavyochangia ukatili kwani wengine kupigwa na wapenzi wao ni upendo," alisema Dk Mbwambo.

Naye, Daktari bingwa na mhadhiri wa Muhas, Dk Samwel Likindikoki alisema kuwa kuna tafiti ndogo ndogo zinazoonesha hali ya watu kutaka kujiua zipo juu kutokana na msongo wa mawazo.

Amesema kuwa madhara wanayoyapata watu wanaofanyiwa ukatili husababishiwa msongo wa mawazo na huduma zinazostahili hawazipati.

"Tunatoa mapendekezo kwa serikali kuhakikisha kuna mpango kazi wa kitaifa wa kushughulikia afya ya akili pia kuendelea kutoa elimu juu ya afya ya akili na namna jamii itaepuka sonona na kutaka kujiua kwa kuwa na njia bora za kushughulikia matatizo yanayowakabili," amefafanua Dk Likindikoki.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi, Muhimbili Prof.Bruno Sunguya. Akimkaribisha DK. Nandera Mhando ili kufungua kongamano Hilo.

Dkt.Omary Ubuguyu aliyemwamilisha Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya akizungumza Katika kikao hicho.


Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof Emmanuel Balandya akitoa neno la shukurani.

Post a Comment

0 Comments