Ticker

6/recent/ticker-posts

ALIYEJIFANYA MTUMISHI WA SERIKALI AFARIKI KWA UTATA KIWANDA CHA RADIANT KONGOWE -RPC LUTUMO

 Na Mwamvua Mwinyi, Pwani


Mtu mmoja Andrew Magembe (40-45) ,amefariki dunia wakati akiwa chini ya ulinzi wa polisi, akipelekwa hospital ya rufaa Tumbi kwa ajili ya matibabu baada ya kukutwa akitokwa na povu mdomoni katika kiwanda cha Radiant Kongowe ,Kibaha ,Mkoani Pwani alipokwenda kufanya wizi kwa kujifanya ni mtumishi wa Serikali akiwa na mwenzake.

Aidha mtoto wa miaka mitatu Salum Sadiki mkazi wa kijiji cha Maneromango Kisarawe amefariki kwa kuzama kwenye kisima cha maji.

Kamanda wa polisi Mkoani Pwani, Pius Lutumo alithibitisha kutokea kwa matukio hayo.

Alieleza, Jeshi la polisi lilipokea taarifa kutoka kiwanda hicho kinachojihusisha na utengenezaji wa vipodozi kuwa kuna watuhumiwa wawili ambao wamejitambulisha watumishi wa Serikali.

"Polisi walifika kwa haraka katika eneo hilo na kuwakuta Watuhumiwa hao ambapo Andrew akiwa amelala chini akitokwa povu mdomoni."":;baada ya watuhumiwa wote wawili kuchukuliwa na polisi Andrew alifikishwa Tumbi kisha kufariki akiwa anapatiwa matibabu"alifafanua Lutumo.

Lutumo alieleza, awali mtuhumiwa huyo akiwa na mwenzake Michael Gerald (40) mkazi wa Kigamboni walifika katika ofisi za kiwanda na kujifanya watumishi wa idara ya mahakama wakiwa na barua feki ya kuomba mchango wa kufiwa na mtumishi mwenzao wa mahakama na barua feki ya utambulisho wa kifo hicho.

"Ambapo katika mahojiano walibainika kuwa ni matapeli na kuwekwa chini ya ulinzi na askari walinzi wa kiwanda hadi polisi walipofika na kuwachukua"alifafanua Lutumo.

Kamanda huyo alieleza, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospital ya Tumbi kwa uchunguzi wa daktari na mtuhumiwa Michael Gerald anashikiliwa na Jeshi la polisi na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.

Lutumo alisema kwamba, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa watuhumiwa hao walikwisha kufanya wizi wa udanganyifu huo katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro.

Akielezea kuhusiana na mtoto kufia kisimani alibainisha, mtoto huyo akiwa na mwenzake aitwaye Falhia Jumanne (2) walikuwa wakicheza pembezoni mwa kisima chenye urefu wa futi 12 kisha kuzama kwenye kisima hicho.

Wakati huo huo, jeshi hilo linawashikilia Watuhumiwa 16 kufuatia kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Alisema, huko kiwanda cha Kairuki pharmaceutical Ltd kinachojihusisha na utengenezaji wa dawa za binadamu Zegereni,walinzi wa zamu wakiwa kazini walivamiwa na kundi la watu watano kisha kunyanyang'anywa silaha moja aina ya short gun protector yenye namba za usajili A09603 iliyokuwa na risasi 12 ikitumiwa na mlinzi Leo Komba.

Lutumo alieleza, mara baada ya kupata taarifa hiyo akiwa na maafisa wenzake na askari wa vyeo mbalimbali walifika eneo la tukio kwa haraka na kuanza msako mkali kisha kufanikiwa kuipata silaha hiyo maeneo ya karibu na kiwanda hicho baada ya wahalifu hao kujaribu kuwashambulia askari polisi na kuzidiwa nguvu kisha kuitupa silaha na kukimbia.

Hata hivyo, Watuhumiwa 16 walikamatwa kuhusiana na tuhuma hiyo na hatua hatua za kiupelelezi zinaendelea.



Post a Comment

0 Comments