SERIKALI YASISITIZA UBUNIFU NA MATUMIZI YA TEHAMA KUINUA UBORA WA ELIMU
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Serikali imesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia na ubunifu wa kisasa katika kuboresha utoaji wa elimu nchini, sambamba na kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu, maadili na miundombinu ya shule.
Akizungumza jijini Arusha wakati wa mkutano wa maafisa elimu wa mikoa na halmashauri nchini (REDEOA), Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Elimu), Atupele Mwambene, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika sekta ya elimu kwa kuongeza bajeti, kujenga miundombinu na kulipa stahiki za walimu kwa wakati.
“Serikali inaweka mkazo mkubwa katika kutumia teknolojia na mbinu za kisasa kuhakikisha kila mwanafunzi anapata fursa sawa ya elimu. Kila mchango wenu ni muhimu katika kuboresha ubora wa elimu nchini,” alisema Mwambene.
Aliongeza kuwa, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna maeneo yanayohitaji nguvu zaidi ili kufikia viwango vya juu vya ubora wa elimu nchini.
“Tunatakiwa kuhakikisha maeneo yote yanafikia zaidi ya asilimia tisini ya utekelezaji wa malengo yetu. Hili litatuhakikishia usawa na ubora wa elimu kwa wote,” alisisitiza.
Aidha, Mwambene alitoa wito kwa maafisa elimu wa mikoa na halmashauri kuendelea kuimarisha uhusiano wa kazi, umoja, upendo na ushirikiano katika majukumu yao ya kila siku, akisisitiza kuwa kiongozi bora ni yule anayeshirikiana na watumishi wake katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.
“Haipendezi kiongozi anapofika ofisini na watumishi wanatokea mlango mwingine. Tunahitaji viongozi wanaowahamasisha na kuwasikiliza watumishi wao,” alisema.
Kwa upande mwingine, Mwambene aligusia changamoto za maadili na matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia, hasa mitandao ya kijamii, akisema zinahitaji kushughulikiwa kwa pamoja kati ya wazazi, walimu na viongozi wa jamii.
“Vijana wanapaswa kufundishwa matumizi mazuri ya TEHAMA bila kuathiri maadili yao. Teknolojia ni muhimu, lakini ni lazima itumike kwa njia yenye tija,” aliongeza.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuzuia ukatili kwa watoto mashuleni, kuwa na kanzidata sahihi ya watumishi wa elimu na kusimamia nidhamu kazini ili kuongeza uwajibikaji na tija.
Kuhusu mpango wa lishe kwa wanafunzi, Mwambene alisema ni muhimu shule zenye mashamba kutumia fursa hiyo kuzalisha chakula kitakachotumika kwa chakula cha mchana, jambo litakalosaidia kupunguza utoro wa wanafunzi.
“Ni jukumu letu kuhakikisha kila mwanafunzi anapata lishe bora na fursa ya kujifunza katika mazingira rafiki,” alisema.
Mkutano huo wa REDEOA ulihudhuriwa na maafisa elimu wa mikoa na halmashauri mbalimbali nchini, ambapo washiriki walijadili njia bora za kuimarisha nidhamu, matumizi ya teknolojia, ufuatiliaji wa maendeleo ya shule na mbinu za kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia