MAKALLA AHIMIZA USHIRIKIANO UTEKELEZAJI WA MIRADI YA BARABARA, TANROADS YAOMBA BILIONI 20 KWA TAA ARUSHA



Na Woinde Shizza,Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arunsha, Amos Makalla amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, wabunge, wenyeviti wa halmashauri, meya wa jiji pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan ya miundombinu ya barabara.


Makalla alitoa kauli hiyo Machi 9, 2026 wakati akifungua mkutano wa 51 wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali ni muhimu ili kuhakikisha miradi ya ujenzi na uboreshaji wa barabara za lami na changarawe inatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.


Alisema kupitia ushirikiano huo itawezekana pia kutatua changamoto mbalimbali za miundombinu ya barabara katika maeneo tofauti ya mkoa huo pamoja na kulinda maslahi ya wananchi.


Makalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha aliwataka wadau wote kuendelea kujituma katika kutekeleza malengo ya serikali ya kuboresha miundombinu ya barabara chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.


Katika hatua nyingine, ameitaka Tanzania National Roads Agency (TANROADS) kuendelea kutumia mabaraza ya madiwani kama jukwaa muhimu la kupokea changamoto za barabara kutoka kwa madiwani katika kata zao ili kuwezesha kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa miradi.


Alisema kikao hicho pia kinaweza kuazimia barabara zitakazopandishwa hadhi au kujengwa kwa kiwango cha lami, ikiwemo barabara ya kuingia Hospitali ya Wilaya ya Arusha DC, Moshono–Bypass, Karatu–Eyasi pamoja na Longido–Siha ili kupunguza kero za usafiri kwa wananchi.


j

Wakati huo huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Regnard Masawe amesema wakala huo umeiomba serikali kiasi cha shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa uwekaji wa taa katika barabara kuu za jiji la Arusha pamoja na barabara ya mzunguko ya Ngaramtoni.



Alisema mradi huo unalenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara, kupunguza ajali pamoja na kuboresha mandhari ya jiji hilo, huku ukihusisha pia uwekaji wa taa katika barabara ya kuelekea Uwanja wa Ndege wa Arusha na barabara ya Arusha–Moshi ambazo ni miongoni mwa barabara zenye matumizi makubwa ya wasafiri na wafanyabiashara.








About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia