USHIRIKIANO WA SEKTA NI NGUZO MUHIMU KATIKA MAFANIKIO YA AFYA MOJA.
Na Mwandishi wetu ,Morogoro
Mkurugenzi Msaidizi wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Salum Manyatta, amesema kuwa Mpango Mkakati wa Afya Moja umejikita kuhakikisha wananchi wananufaika kuanzia ngazi ya mikoa hadi taifa kupitia utekelezaji shirikishi wa sekta mbalimbali.
Dkt. Manyatta ameyasema hayo Aprili 1, 2026 mkoani Morogoro wakati wa kikao kazi cha tathmini ya Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Afya Moja 2022–2027, kilichoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Afya Moja kwa kushirikiana na Shirika la CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani.
Amesema kuwa lengo kuu la kikao hicho ni kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa mpango huo kwa kuangalia shughuli zote zilizofanyika kuanzia ngazi ya uratibu kati ya taasisi mbalimbali hadi utekelezaji katika ngazi za mikoa na serikali za mitaa.
“Tunachokifanya hapa ni kuainisha kwa kina utekelezaji wa Afya Moja katika sekta zote, ikiwa ni pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara na wadau wa maendeleo, ili kuona nini kimefanyika na nini kinahitaji kuboreshwa. Tathmini hii itakuwa msingi muhimu wa kuandaa Mpango Mkakati ujao utakaoanza mwaka 2028,” amesema Dkt. Salum Manyatta.
Kwa upande wake, Mratibu wa Afya Moja na Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Kizoonotiki kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Gwakisa John, amesema sekta ya afya imeendelea kushirikiana kwa karibu na sekta nyingine kupitia uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika kukabiliana na magonjwa na majanga yanayoathiri binadamu.
Ameeleza kuwa kupitia ushirikiano huo, wizara imekuwa ikishiriki kikamilifu katika ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya mlipuko na yale ya kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, yakiwemo kichaa cha mbwa na kimeta, kwa kushirikiana na sekta za mifugo na mazingira.
“Katika utekelezaji wa Afya Moja, tumekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa mifumo ya ubadilishanaji taarifa serikalini.
Hata hivyo, kupitia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, juhudi zinaendelea kuhakikisha mifumo yote ya serikali inaunganishwa ili iweze kuwasiliana kwa ufanisi zaidi,” amesema Dkt. Gwakisa.
Aidha, ameongeza kuwa sekta ya afya imekuwa ikifanya jitihada za kutafuta rasilimali kupitia njia mbalimbali, ikiwemo maandiko ya miradi, ili kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za Afya Moja unakuwa endelevu na wenye matokeo chanya kwa binadamu na mifugo.
Naye MKuu wa Kitengo cha Afya Moja na Uratibu wa Mradi wa Usalama wa Afya Duniani unaotekelezwa na shirika la CIHEB Tanzania, Dkt. Irene Masawe, amesema kuwa ndani ya siku nne za kikao hicho, washiriki wamefanikiwa kupitia kwa kina maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa mpango huo.
Amesema maeneo yaliyopitiwa ni pamoja na uratibu, ufuatiliaji, utekelezaji pamoja na tafiti, ambapo mradi huo umewezesha tathmini hiyo kufanyika kwa umakini mkubwa na kutoa taswira halisi ya mafanikio na changamoto zilizopo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Wataalam ya Afya Moja katika eneo la Utafiti na Maendeleo , Dkt. Maurice Mbunde kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili amesema kuwa tathmini hiyo imeonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo.
Amebainisha kuwa ushirikiano madhubuti chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Afya Moja kwa kiwango cha kuridhisha.
Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha mipango mikakati inafanyiwa tathmini ya mara kwa mara ili kuongeza tija, ufanisi na ubora wa huduma za afya pamoja na usimamizi wa majanga nchini.
@ciheb_tanzania
@who_tanzania
@fao
@wizara_afyatz
@elimu_ya_afya






0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia