RAIS DKT. MWINYI AZINDUA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026, ASISITIZA AMANI, UZALENDO NA UWAJIBIKAJI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Watanzania kulinda, kuimarisha na kudumisha Muungano wa Tanzania, amani, utulivu na umoja wa kitaifa kama msingi wa maendeleo endelevu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 02 Aprili , 2026 wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 uliofanyika Uwanja wa Gombani, Pemba.
Aidha, Rais Mwinyi amesema taasisi zote nchini na wananchi kwa ujumla wana wajibu wa kuheshimu utu, haki, usawa na utawala wa sheria ili kuendeleza mshikamano wa Taifa.
Ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru unaendelea kuwa chombo muhimu cha kuhamasisha uzalendo, uwajibikaji na mapambano dhidi ya maadui wa maendeleo wakiwemo umasikini, ujinga na maradhi.
Vilevile, amewahimiza Watanzania kupinga ubaguzi wa aina yoyote na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na rushwa, dawa za kulevya na magonjwa kama UKIMWI na malaria.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya, kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya na kupunguza maambukizi ya malaria, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kufanikisha maendeleo ya Taifa.
Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake katika Mkoa wa Kusini Pemba na unatarajiwa kufikia kilele chake Oktoba 14, 2026 mkoani Rukwa, ukiwa na kaulimbiu: “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane.”
.jpeg)


0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia