SERIKALI YAONGEZA BAJETI YA OFISI YA MWANASHERIA MKUU HADI BILIONI 61.9



Na Woinde Shizza, Arusha

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesema kuwa ongezeko la bajeti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufikia shilingi bilioni 61.913 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 limetokana na utendaji bora wa taasisi hiyo pamoja na kuongezeka kwa imani ya Serikali katika majukumu yake ya kisheria.

Johari alitoa kauli hiyo Aprili 27, 2026 jijini Arusha wakati akizungumza katika Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo, ambapo alieleza kuwa ongezeko hilo la takribani asilimia 49 litaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kulinda maslahi ya Taifa.

Aidha, aliwataka watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kuzingatia maadili, uwajibikaji na nidhamu katika utendaji wao wa kazi, akisisitiza kuwa mafanikio ya taasisi yoyote ya umma yanategemea uwajibikaji wa watumishi wake.

Katika mkutano huo, wajumbe walifanya uchaguzi wa viongozi wa Baraza la Wafanyakazi, ambapo William Mudogo alichaguliwa kuwa Katibu wa Baraza, huku Fey Sadalla akichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi. Uchaguzi huo ulilenga kuimarisha uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji miongoni mwa watumishi.

Akitoa maoni kwa niaba ya wafanyakazi, Katibu wa Baraza hilo, William Mudogo, alisema licha ya maboresho ya mazingira ya kazi, suala la mishahara bado ni changamoto inayohitaji kipaumbele kutoka Serikalini.

“Mishahara ni msingi wa kuongeza morali na ufanisi kazini. Tunaomba Serikali iangalie upya suala hili,” alisema Mudogo.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Samweli Maneno, alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, ofisi hiyo ilipokea shilingi bilioni 27.159, sawa na asilimia 57 ya bajeti iliyoidhinishwa.

Alieleza kuwa fedha hizo zilitumika katika shughuli mbalimbali za uendeshaji na miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa jengo la ofisi jijini Arusha, huku akibainisha kuwa mafanikio yamepatikana kupitia mikataba zaidi ya 1,000 kati ya 1,324 iliyopangwa.

Katika kuboresha utendaji kazi, watumishi wapya 15 wameajiriwa, 11 wakahamishwa na 14 kupandishwa vyeo, hali iliyofikisha jumla ya watumishi 210. Pia, watumishi 17 wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu ndani na nje ya nchi, huku wengine 192 wakipatiwa mafunzo ya muda mfupi ili kuongeza ufanisi kazini.




Baraza hilo pia lilipendekeza Serikali kuanzisha na kuimarisha ofisi za Mwanasheria Mkuu katika mikoa mbalimbali ikiwemo Kagera, Mtwara, Tanga na Mbeya ili kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia