TUTAHAKIKISHA KUWA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI INAKUWA CHACHU YA KUFIKIA MALENGO YA DIRA 2050” – MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo, wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serkali kilichofanyika tarehe 27 Aprili, 2026 Jijini Arusha.
“Tutahakikisha kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inakuwa chachu ya kufikia malengo ya Dira 2050.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza hilo, Mhe. Johari ameeleza kuwa Dira ya Taifa 2050 inalenga kuwa na Utumishi wa umma unaowajibika, hivyo Matarajio ni kuwa na Utumishi wa Umma unaofanya kazi kwa ufanisi, uwajibikaji, uadilifu, uwazi na wenye kupambana na rushwa.
“Ni dhahiri kuwa, Mabaraza ya wafanyakazi ni nyenzo muhimu kwa ustawi wa watumishi, taasisi na Taifa katika kufikia malengo ya DIRA 2050.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Mhe. Johari Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuipatia Rasilimali na vitendea kazi mbalimbali vinavyowawezesha Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutekeleza Majukumu yao kwa urahisi.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutumia vyema muda wa kazi kwa kutekeleza majukumu yake kwa bidii na weledi, ili kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na kisheria, kupitia utoaji wa huduma za kisheria kwa ubora unaotakiwa na ufanisi na tija inayotarajiwa kwa wadau mbalimbali.
“Naamini katika kikao hiki, mtatoka na maamuzi yatakayoiwezesha Ofisi hii kusonga mbele zaidi.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa bajeti wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya Mikataba ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa 2,324 ilifanyiwa upekuzi kati ya mikataba 2,000 iliyokuwa imepangwa kufanyiwa upekuzi ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 16 ya utekelezaji.
Pia, Mhe. Maneno ameeleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanikiwa kufanya upekuzi wa Hati za Makubaliano (Memorandum of Understanding) 396 kati ya 600 iliyokuwa imepangwa ambapo ni sawa na asilimia 66 ya utekelezaji.
“Mikataba iliyofanyiwa upekuzi ilihusisha masuala ya ununuzi na ujenzi, na ukarabati wa majengo, utoaji huduma za jamii kama vile ujenzi wa shule, hospitali na barabara, huduma za kitaalam, na ununuzi wa bidhaa.” Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilipokea jumla ya maombi ya ushauri 1,897 kutoka kwenye Wizara, Idara zinazojitegemea, Mashirika ya Umma, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na wadau wengine.
Vilevile, ameeleza kuwa Ofisi ilifanikiwa kuratibu na kufuatilia Utekelezaji wa Majukumu ya Kamati za Kudumu za Ushauri wa Kisheria za Mikoa na Wilaya kwa kuzindua na kuendesha Kliniki bure za Ushauri wa Kisheria katika Mikoa ya Manyara, Simiyu na Dar es Salaam na Wilaya zake.
Sambamba na hilo Mhe. Maneno amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kuboresha Mazingira ya kufanyia kazi kwa kuunganisha Mfumo wa OAG-MIS na Mifumo ya Kesi (Case Management Systems) ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Mahakama ya Tanzania.
Awali, akiwasilisha Risala ya Wafanyakazi, Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Rashidi Kigalu ameushukuru na kuupongeza uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuboresha mazingira na maslahi ya Watumishi, yanayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
“Kwa niaba ya Watumishi natoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu, Naibu Mwanasheria Mkuu na Menejimenti kwa ujumla kwa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi kwa watumishi.” Amesema Bw. Kigalu
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wamefanya uchaguzi kwa kuwachagua Bw. William Mudogo kuwa Katibu na Bi. Fay Grace Sadallah kuwa Katibu Msaidizi wakichukua nafasi hizo baada ya Bi. Beatrice Nzobonaliba na Bw. Hassan Nkya waliomaliza muda wao.










0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia