UCHAGUZI WA ALAT KUFANYIKA ARUSHA APRILI 22–23, 2026
Na Woinde Shizza, Arusha
JUMUIYA ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) imetangaza rasmi uchaguzi wa viongozi wake wa ngazi ya Taifa utakaofanyika Aprili 22 hadi 23, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC, jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT, Thomas Vungwa, amesema uchaguzi huo utahusisha nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Mwenyekiti wa WASEMI, Makamu Mwenyekiti wa WASEMI pamoja na Kamati Tendaji ya WASEMI.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Katiba ya ALAT ya mwaka 2014 pamoja na kanuni za kudumu za mikutano na uchaguzi wa viongozi wa ALAT za mwaka 2009 (kanuni ya 27 hadi 34), ninatangaza rasmi kuitishwa kwa uchaguzi wa viongozi wa jumuiya,” amesema Vungwa.
Ameeleza kuwa uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa ALAT ngazi ya Taifa utafanyika kwa mujibu wa kifungu hicho, ambapo waombaji watahitajika kujaza fomu maalum za kuwania nafasi hizo.
Amesema kila mwombaji atapaswa kuungwa mkono na wajumbe wawili kutoka kila kanda, huku zoezi la uchukuaji wa fomu likianza Aprili 17 hadi 21, 2026.
“Fomu za maombi zitawasilishwa katika ofisi ya Sekretarieti ya Jumuiya kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana Aprili 21, 2026 katika Ukumbi wa AICC,” amesema.
Ameongeza kuwa zoezi la uchujaji wa wagombea litafanyika Aprili 21, huku kampeni za kujinadi na uchaguzi wenyewe ukifanyika Aprili 22, 2026.
Vungwa amesisitiza kuwa wagombea wote wanapaswa kuzingatia taratibu na miongozo iliyotolewa kwa makatibu na wenyeviti wa ALAT katika ngazi za mikoa.
Aidha, amesema ALAT hufanya uchaguzi wa viongozi wake kila baada ya miaka mitano na kutoa wito kwa wanachama wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali huku wakizingatia sheria na kanuni zilizowekwa.





0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia