UHURU WA VYOMBO VYA HABARI WAZIDI KUDORORA TANZANIA



Na Woinde Shizza, Arusha

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Anna Henga, amesema hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini imeendelea kudorora kwa kiwango kikubwa, hali inayotia wasiwasi kuhusu mustakabali wa tasnia hiyo.


Dkt. Henga alitoa kauli hiyo leo Aprili 29, 2026 jijini Arusha wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ambapo wadau wa sekta ya habari walikutana kujadili hali ya uhuru wa vyombo vya habari na mwelekeo wake nchini.


Alisema licha ya Tanzania kufanya tathmini ya haki za binadamu inayojumuisha zaidi ya haki 60 kila mwaka, sekta ya habari imeendelea kuwa miongoni mwa zilizoathirika zaidi.


“Katika mwaka uliopita, ambao ulikuwa na muktadha wa uchaguzi, kulikuwa na matukio mengi yaliyoathiri wanahabari, ikiwemo kukamatwa, kupotea katika mazingira ya kutatanisha na hata matukio ya mauaji,” alisema.


Aliongeza kuwa katika kipindi hicho, wanahabari kadhaa walikamatwa kinyume cha taratibu huku wengine wakishikiliwa bila kufikishwa mahakamani, jambo linalokiuka misingi ya haki.


Aidha, alieleza kuwa kufungwa kwa huduma za intaneti hasa wakati wa uchaguzi kulikuwa kikwazo kikubwa kwa vyombo vya habari vya mtandaoni na kuathiri upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.


“Unapofunga intaneti, unazuia kabisa uwezo wa vyombo vya habari kufanya kazi. Hili ni pigo kubwa kwa uhuru wa habari katika zama za kidijitali,” alisisitiza.


Dkt. Henga pia alibainisha kuwa vyombo kadhaa vya habari vilifungiwa kwa nyakati tofauti, hali iliyodhoofisha tasnia hiyo na kuendelea kuripotiwa hata katika robo ya kwanza ya mwaka huu.


Akizungumzia ubunifu wa wanahabari, alisema hauwezi kustawi katika mazingira ya hofu na vitisho, akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mazingira salama na huru ili wanahabari waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.


Kuhusu mfumo wa kisheria, alisema licha ya Katiba ya Tanzania, hususan Ibara ya 18, kulinda uhuru wa kutoa na kusambaza taarifa, bado kuna changamoto katika baadhi ya sheria zinazohusu maudhui na vyombo vya habari.


Alisisitiza umuhimu wa kufuata misingi ya haki (due process), akitaka wanahabari na vyombo vya habari vinaposhitakiwa kupewa nafasi ya kusikilizwa kabla ya kuchukuliwa hatua zozote.


Akizungumzia mahusiano kati ya serikali na vyombo vya habari, Dkt. Henga alisema bado kuna mvutano, huku baadhi ya viongozi wakiviona vyombo vya habari kama wakosoaji badala ya washirika katika maendeleo.


Alishauri serikali kuviona vyombo vya habari kama chombo muhimu cha kujitathmini na kuboresha utawala, akisisitiza kuwa ukosoaji ni sehemu ya ujenzi wa taifa lenye uwajibikaji.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia