ELIMU YA FEDHA YAONGEZA MATUMAINI ARUSHA: WANANCHI WAPATA MWANGA WA KIUCHUMI
Na Woinde Shizza,Arusha
Halmashauri ya Jiji la Arusha imezindua rasmi zoezi la uhamasishaji wa wananchi kuhusu fursa mbalimbali zilizopo ndani ya jiji hilo, likihusisha taasisi za serikali pamoja na taasisi za kifedha, ikiwa ni hatua muhimu ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kata ya Terrat na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi waliopata fursa ya kujifunza na kuelimishwa kuhusu upatikanaji wa mikopo, uwekezaji pamoja na usimamizi bora wa fedha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Maendeleo wa Jiji la Arusha, Shabani Manyama, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji, amesema kuwa halmashauri imetenga zaidi ya shilingi bilioni 5.3 kwa ajili ya mikopo kwa wananchi katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesisitiza kuwa fedha hizo zipo tayari kutolewa, hivyo wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo ili kuboresha maisha yao.
Aidha, wananchi wamehimizwa kuwa makini wanapochukua mikopo kwa kuhakikisha wanatambua malengo ya mkopo kabla ya kukopa, kufanya tathmini halisi ya biashara zao, na kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa,huku ikielezwa wazi kuwa mkopo siyo fedha ya matumizi holela bali ni nyenzo ya kukuza uchumi.
Miongoni mwa wananchi walioshiriki katika uzinduzi huo, Elizabeth Shirima amesema fursa hizo zimekuja kwa wakati muafaka na zina matarajio ya kuwasaidia wananchi wengi kujikwamua kimaisha, hasa kutokana na uwepo wa mikopo isiyo na masharti magumu kama ilivyokuwa awali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilaitairo, Kata ya Terrat, Aron Lukumai, amesema wananchi wamepokea kwa furaha ujio wa fursa hizo, akibainisha kuwa changamoto kubwa hapo awali ilikuwa ni ukosefu wa uelewa.
Ameongeza kuwa kusogezwa kwa huduma karibu na wananchi kutarahisisha upatikanaji wa mikopo na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.
Kwa ujumla, zoezi hilo limepokelewa kwa mwitikio chanya, huku likitarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Jiji la Arusha kupitia matumizi sahihi ya fursa zinazotolewa.






0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia