WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUENDANA NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA
Na Woinde Shizza, Arusha
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kihabari ya Media Brains, Jesse Kwayu, amesema kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwa kujifunza mbinu mpya za uandishi wa habari za mtandaoni ili kuendelea kutoa taarifa sahihi na zenye tija kwa jamii.
Kwayu ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na kampuni hiyo kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha, yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuandika na kuripoti habari za mtandaoni katika mazingira ya sasa ya maendeleo ya teknolojia.
Amesema kuwa kwa sasa tasnia ya habari imebadilika kwa kiasi kikubwa na kuhamia zaidi katika majukwaa ya mtandaoni, hali inayowalazimu waandishi wa habari kujifunza mbinu mpya za uandishi pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili unde (AI) katika ukusanyaji na uchakataji wa taarifa.
Aidha, amesema mafunzo hayo pia yamelenga kuwasaidia waandishi wa habari kutambua na kuchambua taarifa za uongo na uzushi ambazo zimekuwa zikisambaa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya kidijitali.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema yamekuja wakati muafaka kutokana na kuongezeka kwa taarifa zisizo sahihi katika jamii, hali inayotokana na kukua kwa teknolojia na urahisi wa kusambaza habari kupitia mitandao ya kijamii.
“Bila kuwa na maarifa ya kitaaluma ni ngumu kujua taarifa husika ni ya kweli au ya uongo, lakini mafunzo haya yametoa elimu kwa waandishi kutumia zana za kiteknolojia za kupima na kubaini habari sahihi na zile za uongo,” amesema Ashura Mohamed, mwandishi wa habari kutoka Radio 5.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu, amesema waandishi waliopata mafunzo hayo wanatarajiwa kuwa mfano kwa wengine kwa kuhakikisha wanazingatia maadili ya taaluma na kuepuka kusambaza habari zisizo na uthibitisho katika majukwaa ya mtandaoni.













0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia