BREAKING NEWS

Wednesday, April 17, 2024

WANAWAKE VIONGOZI WAHIMIZWA KUJILINDA DHIDI YA KUCHAPISHA MAUDHUI MABAYA MITANDAONI

 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Youth Environmental Justice and Gender equality Bi.Philomena Mwalongo akizungumza wakati wa mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19. Mafunzo hayo ya siku moja yamegfanyika katika ukumbi wa hoteli ya Kingsway mkoani Morogoro



WANAWAKE viongozi na vijana wanasiasa wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa tija kwa lengo la kupeana taarifa na kuondokana na matumizi mabaya yenye kuleta athari hasi kwa vijana wakike wanaotarajia kuwa viongozi wa baadae.


Wito huo umetolewa Aprili 16,2024 mkoani Morogoro na Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Ruth John wakati akifungua mafunzo ya ulinzi wa taarifa na usalama yaliyoandaliwa na Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) kwa kushirikiana na Taasisi ya YOGE pamoja na Article 19.


Alisema kuwa miaka ya sasa wanasiasa na viongozi wanawake wamekuwa wakikumbwa na ukatili na mashambulizi mitandaoni kutoka kwa watu wasio na mapenzi mema kwa nchi.


"Wanawake ni jeshi kubwa sana na ndio taswira ya taifa na mwanamke huyu anapochafuliwa katika mitandao ataathiri jeshi kubwa ambalo liko nyuma yake hasa vijana wanaochipukia kuwa viongozi hapo baadae", alisema.


Aidha alieleza kuwa mafunzo hayo yanakwenda kujenga uwezo na uelewa kwa wanawake kuhusiana na kutunza taarifa zao pamoja na namna ya kukabiliana na kudhibiti vitendo vya ukatili jambo ambalo litaweka uhakika wa kuwaweka salama wakati wote.


Pamoja na hayo Mhe.Ruth aliwaasa viongozi na wanasiasa kuwa makini na maudhui yao wanayoyaweka mitandaoni,ambapo amebainisha kuwa kukosekana kwa umakini na weledi husababisha mianya na matumizi mabaya ya maudhui ambayo yanaweza kuwaathiri wao na jamii yao.


Pamoja na hayo alitoa pongezi kwa Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE),YOGE pamoja na Article 19 kwa kuanzisha mafunzo hayo ambayo yataleta matokeo chanya kwa viongozi.


Kwa Upande wake Mwanzilishi wa Shirika la (TAMCODE) Bi.Rose Ngunangwa alisema wameamua kuanzisha mafunzo hayo baada ya kugundua kuwa kuna changamoto kwa wanawake kushambuliwa hasa kipindi cha uchaguzi unapokaribia jambo ambalo linadhoofisha nguvu zao katika kuwania nafasi za uongozi.


"Wanawake bado hawajapata ujuzi wa kutosha kwenye matumizi ya mitandao katika kujiwezesha kiuchumi ndio maana sisi TAMCODE,YOGE pamoja na Article 19 tumeona tuanze kuwajengea uwezo wanawake madiwani kwa ukanda wa pwani ili kuwawezesha wanapoelekea katika uchaguzi watumie mitandao kunadi sera zao", alieleza.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Youth Environmental Justice and Gender equality Bi.Philomena Mwalongo alisema mafunzo hayo yamelenga kuwainua wanawake na vijana katika nyanja ya kiuchumi,Siasa pamoja na Teknolojia.


"Tulifanya tafiti tukagundua kuna ombwe kubwa katika ushiriki wa Wanawake viongozi na wanasiasa katika kutambua matumizi salama ya mitandao,na sio tu kujinufaisha wanawake binafsi waliohudhuria hapa Ila kuwagusa wanawake wengine ambao hawapo hapa", alisema


Vilevile Diwani wa kata ya Mji Mpya,Manispaa ya Morogoro Bi.Emmy Kiula ametoa shuhuda ya kuchafuliwa mtandoni ambapo ameeleza kuwa jambo hilo halipendezi kwani linaondoa imani kwa wananchi ambao wamempa dhamana ya uongozi.


"Serikali iangalie sasa kwa wale ambao watabainika sheria iwe kali, watu waadhibiwe na waache tupo katika ulimwengu wa maendeleo,lakini sasa tunapoitumia tofauti mitandao inakatisha tamaa,mtu anapoitumia mitandao kutoa lugha chafu haipendezi,utu wa mtu ni kuheshimiana,"Bi.Emmy alieleza.


Mafunzo hayo,yamejuimuisha wanawake viongozi na vijana wanasiasa katika ukanda wa Mkoa wa pwani,Dar es Salaam pamoja na Morogoro yamejikita hasa kuwainua wanawake katika nyanja ya Uchumi,kisiasa na kiteknolojia kwa kuwajengea uwezo katika masuala hayo.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates