Ticker

6/recent/ticker-posts

WATAKIWA KUONDOA HOFU WANAPOANZISHA BIASHARA




Na Mwandishi wetu 


Wanawake na Wasichana wameshauriwa kuondoa hofu wanapotaka kuanzisha biashara ili kujinyanyua kiuchumi kupitia fursa mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi na madini.


Ushauri huo umetolewa na wataalam mbalimbali katika kongamano la Wanawake na Wasichana Kanda ya Ziwa linaloitwa CHANUO SUMMIT lenye kauli mbiu isemayo JISUKE UISUKE DUNIA lililoratibiwa na Kampuni ya Jambo Group.


Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara, Kilimo na Viwanda Mkoa wa Shinyanga (TCCIA) Jonathan Manyama amesema hofu ndiyo inayokatisha tamaa Wanawake na Wasichana wanapotaka kuanzisha biashara hivyo kuwashauri wasiangalie nyuma.


“Kongamano hili limekuwa zuri kwa kuwaleta pamoja wafanyabiashara wazoefu na wale wanaotaka kuanza wajifunze zaidi hivyo Jambo FM wamefanya kitu kikubwa sana”,amesema Manyama.


Naye Meneja wa Jambo Media, Nickson George amesema uanzishwaji wa kongamano hilo na neno Chanuo umebeba dhamira kuu kwa wanawake na wasichana kutengua maisha yao kwa kupitia fursa, hivyo kwa kanda ya Ziwa wanahitaji kupata elimu zaidi ikiwa leo wamekuja na mada tatu muhimu za kuwajenga ambazo ni Kilimo, Uvuvi na Madini.


Amesema kongamono hilo ni mwendelezo wa makongamano mengine ya kimataifa kuwakutanisha wafanyabiashara Wanawake na Wasichana walio wazoefu na chipukizi kwa kukutanisha nchi za Afrika mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda na Ethiopia.


“Kanda ya ziwa katika utafiti uliofanyika ina watu takribani Milioni 17 ambao kila siku wana mahitaji, tumeona kuchukua fursa ya kuwafundisha Wanawake na Wasichana wanaopitia changamoto nyingi za kuweza kujikomboa kiuchumi na kutumia fursa zilizopo”,amesema George


Naye Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi amesema jeshi hilo litaendelea kuimarisha usalama kwa Wanawake na Wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili kupitia dawati la jinsia


Hellen Samson mkulima wa zao la mkonge kutoka wilayani Kishapu amesema ameweza kunufaika kupita zao hilo na soko lipo ambapo anawashauri wanawake wenzake na wasichana kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo na biashara ili wajinyanyue kimaisha kwani zao hilo halina changamoto kubwa kama wanavyofikiria.


Bwana shamba kutoka kampuni ya Burton Tanzania inayojishughulisha na kilimo cha nyanya Bernad Musiba amesema zao hilo kwa kanda ya ziwa linapata soko kubwa changamoto inayowafanya wafanyabiashara waliogope namna wanavyopata changamoto na kuanza bila kufanya utafikiti wa kina. 


Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria kongamano hilo wamesema kongamano hilo limewawezesha kubadilishana mawazo na kujifunza kwa kuondoa hofu na kila mwaka liwepo kongamano hilo wajifunze zaidi.



Meneja mkuu Jambo Media, Nickson George akielezea lengo la kongamano la Wanawake na Wasichana Kanda ya Ziwa linaloitwa CHANUO SUMMIT

Post a Comment

0 Comments