BREAKING NEWS

Sunday, February 6, 2011

JK NAUNGA MKONO DOWANS ISILIPWE

RAIS Jakaya Kikwete jana alitumia maadhimisho ya miaka 34 ya CCM kuvunja ukimya na kuzungumzia sakata la malipo kwa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans kiasi cha Sh94 bilioni akisema amaunga mkoTanesco isilipe deni la Dowans.

"..Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka Tanesco ilipe..," alisema Rais Kikwete akizungumzia sakata hilo.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete kuhusu Dowans ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu na Watanzania, ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakitoa maoni mbalimbali,huku baadhi yao wakienda mahakamani kupinga kampuni hiyo isilipwe.

Akihutubia wananchi katika kilele cha Sikukuu ya kuzaliwa kwa CCM, ambazo kitaifa zilifanyika mkoani Dodoma jana Kikwete alisema ameamua kusema wazi baada ya kupata shinikizo kutoka kwa watu mbalimbali waliosema kuwa amekuwa kimya juu ya Dowans.

“Wapo wanaosema niko kimya au nashindwa kuchukua hatua, kwa sababu marafiki zangu wamehusika. Nawalinda. Kwa sababu hiyo, nikaona nami nisema angalau watu wanisikie, lakini sina la ziada ni yale yale yaliyokwishasemwa.

“Msemo wa wahenga wa akutukanae hakuchagulii tusi hapa umetimia. Napenda kuwahakikishia wana-CCM na wananchi wenzangu kuwa, sina uhusiano wowote wa kimaslahi, kwa namna yoyote ile na kampuni ya Dowans,” alisema Kikwete.

Rais Kikwete alisema hakutaka kuzungumza kuhusu Dowans kwa kuwa tayari lilikuwa limeshatolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati .

“Sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu viongozi wenzangu wameelezea kwa ufasaha uamuzi wa Kamati Kuu na ule wa kikao cha pamoja cha Wabunge wa CCM,” alisema Rais Kikwete.

Alisema kuwa taarifa ya kutaka Tanesco iilipe Dowans Sh94 bilioni imeshtua wengi na kwamba yeye baada ya kupata taarifa hiyo aliuliza na kupewa ushauri mbalimbali.

“ Wapo waliosema lazima tulipe, wapo waliosema tusilipe, wapo waliosema tusiharakishe kulipa kwani kuna uwezekano wa kutokulipa kwa kutumia sheria,” alisema na kuongeza

“ Uamuzi wangu ukawa tusiharakishe kulipa, tutafute njia za kuepuka katika kulipa. Ndiyo maana ya taarifa ya Chiligati na ile ya Waziri Mkuu,” alisema Kikwete.

Alisema kuwa ni mzigo mkubwa kwa Tanesco kuilipa Dowans, hivyo ifanyike kila njia ili kuepuka kulipa deni hilo.

“ Tumewataka wanasheria wetu wasaidiane na wale wa Tanesco kuhakikisha hilo halitokei. Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka Tanesco ilipe," alisema na kusisitiza:

"Kauli za mimi kuhusika na Dowans inanishangaza, maana nisingeamua hivyo katika Kamati Kuu(CC) na Kamati ya Wabunge wa CCM. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi”alisema Kikwete."

Alisema kutokana na ukimya wake maneno mengi yalisemwa ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na kampuni hiyo Dowans na kufafanua kwamba jambo jingine lililomfanya kuzungumza kuhusu Dowans ni kauli kwamba hawezi kuzungumza kwa kuwa kampuni hiyo inahusishwa na marafiki zake.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates