BREAKING NEWS

Thursday, February 3, 2011

MKURUGENZI OXFAM AZURU MERERANI




Mkurugenzi wa Oxfam,Jim Claken akitazama madini ya Tanzanite kwenye ofisi ya Nickson Gem Cut mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro


WAKAZI wa mji ndogo wa Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wametakiwa wayathamini na kuona fahari kutokana na madini ya Tanzanite kuwa kwenye mji huo pekee dunia.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Oxfam,Jim Claken,wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini kwenye migodi ya Tanzanite wilayani Simanjiro.

Claken alisema madini hayo yanapatikana Mirerani peke yake na amekuwa akisoma kwenye mtandao habari za madini hayo ya Tanzanite na amefurahi kufika kwenye machimbo hayo na kujionea kwa macho.

Mkurugenzi huyo wa shirika hilo lenye makao makuu yake nchini Ireland aliongozana na Mkurugenzi wa shirika hilo nchini,Monica Gorman,William Stattey na Peter Anderson na mwenyeji wao Amani Mustapha ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la Haki Madini.

Claken alisema amejifunza mambo mbalimbali ambayo hakuwa anayatambua ikiwemo namna madini hayo yanavyochimbwa na akirudi nchini Ireland ataelezea kwa ufasaha mazingira ya Tanzanite.

Naye Mkurugenzi wa shirika la Haki Madini Mustapha alisema lengo la ziara hiyo ni kutembelea,kujifunza na kujionea kazi mbalimbali zinazofadhiliwa na shirika la Oxfam.

Mustapha alisema zaidi ya kutembelea machimbo ya Tanzanite ugeni huo wa Oxfam pia ulitembelea Tanzanite Walking Culture Tourism,Nickson Gem Cut na vikundi vya Sewomi Saccos na Tujinyanyue.

Alisema kabla ya kufika mji mdogo wa Mirerani,ujumbe huo ulitembelea Loliondo wilayani Ngorongoro kwa ziara ya siku mbili ambapo walifika kwenye hifadhi za mbuga za wanyama.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates