WADAU WATAKIWA KUUNGANA NA KUSHIRIKIANA ILI KUTOKOMEZA MIGOGORO YA ARDHI




 Na Woinde Shizza, ARUSHA 


Wadau wametakiwa kuungana na kushikamana kwa pamoja ili kutokomeza Migogoro ya Ardhi ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikisababisha uvunjifu na ukiukwaji wa haki za binadamu, utawala bora na wa kisheria nchini huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto.

Hayo yameelezwa katika  mjadala uliowakutanisha waandishi wa habari,Asasi za Kiraia ,wanaharakati wa haki za binadamu,wanataaluma, umma wa watanzania na wanawake ambao ndiyo waathirika wakubwa wa Migogoro hiyo kupitia mtandao wa Zoom Meeting uliokuwa na lengo la kutafuta Suluhu ya athari za Migogoro ya ardhi hususani Mgogoro wa Ngorongoro na Loliondo kwa kutoa mapendekezo ili kupata Suluhu kwa ajili ya ustawi wa jamii na Taifa, ulioandaliwa na shirika la Civic and Legal Aid Organization (CILAO) kwa kushirikiana na wadau na Watetezi wa haki za binadamu.

Mmoja wawashiriki hao aliejitambulisha kwa jina la Nailejileji Tipap  alizitaka taasisi mbalimbali za kiraia zikiwemo za haki za binadamu kushikamana kwa pamoja, kupaza sauti kwa jamii ili kutokomeza migogoro inayopelekea kutokea kwa mazingira duni kwa waathiriwa sambamba na vitendo vya ukatili kwenye jamii.

Katika Mjadala huo vilisomwa vifungu mbalimbali vya sheria ya hifadhi ikiwemo sheria ya Ngorongoro Conservation Area Act Sura namba 284 kifungu cha 6 kinachoelezea kinagaubaga malengo ya kuanzishwa kwa hifadhi hizo na endapo ikivunjwa ni dhahirishahiri inaweza kusababisha athari kwa jamii na Taifa huku waathirika wakuu ni wanawake na watoto.

Mjadala huo ulihitimishwa kwa maadhimio ya kupaza sauti kwa pamoja, kutoa elimu kwa jamii kwa kutumia vyombo vya habari, ili kuonyesha taswira halisi ya madhara ya migogoro ya ardhi katika sekta ya uchumi, elimu, na hata katika huduma za kijamii ili viongozi wa ngazi za juu wasikie na kutafuta mwarobaini wake kwa wakati.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post