Na Woinde Shizza
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye amezindua programu ya Shahada ya Media Anuwai na Mawasiliano kwa Umma katika chuo cha uhasibu Arusha na kuwataka wanafunzi hapa nchini kutumia fursa hiyo kujiendeleza ili kuleta mabadiliko katika tasinia ya habari.
Akizindua kozi hiyo Nape alisema kuwa,kitendo cha kuzinduliwa kwa programu mpya chuoni hapo ni jambo kubwa sana kwa maslahi ya nchi na linapaswa kuigwa na vyuo vingine ili kuweza kupata wataalamu wengi zaidi waliobobea katika fani hiyo.
Nape alisema kuwa,kuwepo kwa programu hiyo katika chuo hicho kutasaidia kupata wataalamu bora na wa kipekee waliobobea na kuondokana na changamoto ya kuwa na wanataaluma katika fani hiyo ambao hawajabobea katika maswala ya habari.
Aidha Waziri Nape aliuomba uongozi wa chuo hicho kufikiria namna ya kuanzisha kozi fupifupi ambazo zitawawezesha wale ambao walishapitia kozi zingine kuweza kujifunza zaidi huku wakiahidi kutoa ushirikiano kwa chuo hicho ili kuhakikisha jambo hilo linafika mbali zaidi.
"Ninakipongeza Chuo cha uhasibu Arusha kwa ubunifu huu wa kuunganisha media Anuwai na mawasiliano kwa umma nafikiri kwa Tanzania kitakuwa chuo cha kwanza na wataalamu watakaopatikana hapa watazingatia sheria na maadili ya taaluma ya habari "
"Vyuo vingi vikiwemo vyuo vikuu vimekuwa vikitoa shahada ya mawasiliano kwa umma pekee, kuunganishwa kwa fani hizi mbili zinazohusiana ni ishara kwamba wataalamu watakaoandaliwa watakuwa bora zaidi"
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Uhasibu Arusha ,Prof Eliamani Sedoyeka alisema kuwa,chuo hicho katika mwaka wa masomo 2023/2024 wanatarajia kuanzisha kozi mpya tano ambapo kati ya hizo kozi za shahada ni nne na moja ya shahada ya Uzamili.
Alisema kuwa ,kuanzishwa kwa kozi hizo kunafanya IAA kuwa na jumla ya kozi 71 ambapo kati ya hizo kozi 16 ni ngazi ya cheti,kozi 17 za stashahada ,kozi 24 za shahada na kwa upande wa shahada ya Uzamili ni kozi 14.
Naye Mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo cha Uhasibu Arusha,Dk Mwamini Tulli alisema kuwa,ubunifu uliofanywa na chuo hicho ni jambo kubwa na linapaswa kuigwa na vyuo vingine kwani kuanzishwa kwa kozi hiyo ni kuona umuhimu wa kutoa fursa kwa vijana wa kitanzania kusoma shahada hiyo muhimu katika tasnia ya habari na mawasiliano.
Aliongeza kuwa, uzinduzi wa shahada hiyo unadhihirisha jinsi chuo hicho kinavyowekeza katika kutoa elimu bora na kukidhi mahitaji ya wakati ,ambapo ametoa wito kwa wazazi pamoja na walezi kukitumia vizuri chuo hicho kuhakikisha wanapeleka watoto wao kujifunza zaidi.