Tumekuja kufanya mapinduzi” — Digingoto afunguka kuhusu Arusha Classic Band
Na Woinde Shizza, Arusha
Bendi mpya ya muziki wa dansi ya Arusha Classic Band imeanza kujizolea umaarufu ndani ya Mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani, huku viongozi wake wakieleza dhamira ya kurejesha hadhi ya muziki wa dansi na kuleta mapinduzi mapya katika tasnia hiyo nchini.
Bendi hiyo ambayo imeanzishwa miezi mitatu iliyopita, imekuwa kivutio kwa mashabiki wa muziki kutokana na ubunifu wa uimbaji, mpangilio wa ala za muziki pamoja na miondoko ya kisasa inayochanganya ladha ya zamani na kizazi cha sasa.
Akizungumza kuhusu safari ya bendi hiyo, Rais wa Arusha Classic Band, Mupendawatu Kambal, alisema wameamua kuingia kwenye tasnia ya muziki wa dansi kwa lengo la kuurudisha muziki huo katika ushindani mkubwa na kuufanya uvutie kizazi kipya.
Alisema kwa muda mrefu muziki wa dansi umekuwa ukipoteza nguvu katika baadhi ya maeneo, hali iliyowasukuma kuanzisha bendi yenye ubora wa kipekee, mafunzo ya kisasa kwa wanamuziki pamoja na burudani inayolenga familia na jamii kwa ujumla.
“Tumekuja kufanya mapinduzi ya muziki wa dansi ndani ya Arusha na Tanzania kwa ujumla ,tunataka watu waone kuwa dansi bado inaweza kuteka soko na kutoa burudani safi yenye maadili, ubunifu na mvuto wa kipekee,” alisema Digingoto.
Kwa upande wake, mmoja wa wanamuziki wa bendi hiyo Robi Matunda aliwataka mashabiki wa muziki wa dansi kujitokeza kwa wingi kushuhudia uwezo na ubunifu wa bendi hiyo mpya inayokuja kwa kasi kwenye tasnia ya burudani.
Alisema Arusha Classic Band imejipanga kutoa burudani ya kiwango cha juu itakayowaacha mashabiki wakiwa na kumbukumbu ya kipekee kila wanapohudhuria maonesho yao.
“Tunawaomba wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla wajitokeze kushuhudia kile tunachokifanya,tumejipanga kuhakikisha mashabiki wanapata burudani bora yenye ladha halisi ya muziki wa dansi,” alisema Robi Matunda.
Kwa mujibu wa viongozi wa bendi hiyo, wameanza maandalizi ya kurekodi nyimbo mpya pamoja na kufanya maonesho katika maeneo mbalimbali mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya kujitangaza zaidi kwa mashabiki wa muziki.
Baadhi ya wadau wa burudani jijini Arusha wamesema ujio wa Arusha Classic Band unaweza kuwa mwanzo mpya wa kuufufua muziki wa dansi katika ukanda wa Kaskazini na Tanzania kwa ujumla kutokana na ari, ubunifu na nguvu mpya walizonazo wanamuziki wake.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia