KISWAHILI KUFUNDISHWA NCHINI URUSI
Na Woinde Shizza,Arusha
Tanzania na Urusi zimekubaliana kutumia lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kufundishwa katika taasisi za elimu ya juu nchini Urusi, ikiwa ni jitihada za Serikali ya Tanzania kuhakikisha lugha hiyo inaongeza idadi ya wazungumzaji duniani pamoja na kuwa chanzo cha fursa za ajira na maendeleo ya kiuchumi.
Makubaliano hayo yamefikiwa kupitia Kikao cha Tatu cha Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Biashara na Uchumi kati ya Tanzania na Urusi kilichowakutanisha viongozi wa serikali, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya uchumi.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Mei 16, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), jijini Arusha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema hatua ya Kiswahili kufundishwa nchini Urusi itasaidia kueneza zaidi lugha hiyo duniani huku ikifungua fursa mpya za kiuchumi, elimu na ajira kwa Watanzania.
Katika kikao hicho pia kulifanyika utiaji saini wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo mkataba wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika taasisi za elimu nchini Urusi. Mkataba huo ulisainiwa kati ya Mtendaji Mkuu wa Baraza la Kiswahili Taifa Bi. Consolata Mushi na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Shirikisho la Urusi, Maxim Reshetnikov.
Aidha, Prof. Mkumbo amesema Tanzania na Urusi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali muhimu zikiwemo viwanda, biashara, miundombinu ya usafirishaji pamoja na usafiri wa anga. Amesema nchi hizo mbili zinaendelea na mipango ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Urusi ili kurahisisha biashara, utalii na uwekezaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amepongeza makubaliano hayo akisema yataimarisha zaidi uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Urusi pamoja na kuitangaza lugha ya Kiswahili katika mataifa mbalimbali duniani.











0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia