TANZANIA, URUSI KUIMARISHA ZAIDI BIASHARA NA UWEKEZAJI
Na Woinde Shizza, Arusha
Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kufanya mageuzi makubwa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia wawekezaji zaidi kutoka mataifa mbalimbali duniani huku ikisisitiza kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi.
Hayo yamesemwa leo Mei 15, 2026 jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo wakati akitoa hotuba katika Jukwaa la Pamoja la Biashara na Uwekezaji lililoandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) katika ukumbi wa Arusha International Conference Centre (AICC).
Jukwaa hilo ni sehemu ya mwendelezo wa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja kati ya Tanzania na Urusi kuhusu biashara na uwekezaji ukiwakutanisha wataalamu na wawekezaji kutoka mataifa hayo mawili.
Katika hotuba yake, Prof. Mkumbo alisema Tanzania na Urusi ni washirika wa muda mrefu waliodumisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kwa zaidi ya miaka 60, akieleza kuwa ushirikiano huo utafungua fursa mpya za biashara, teknolojia na uwekezaji.
“Uhusiano wetu umeendelea kuimarika kwa miaka mingi na sasa tunaelekea katika hatua mpya ya ushirikiano wa kiuchumi wenye manufaa kwa mataifa yetu,” alisema Prof. Mkumbo.
Jukwaa hilo pia limehudhuriwa na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Shirikisho la Urusi, Maksim Reshetnikov ambaye ameongoza ujumbe mkubwa wa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali nchini humo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejidhatiti kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki, yenye uwazi na yanayotabirika kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Dkt. Chaya alisema Tanzania ipo katika kipindi muhimu cha mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kuifanya nchi kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla.
Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu unaochochewa na viwanda, ubunifu na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.
Ameongeza kuwa Serikali inalenga sekta binafsi kuchangia zaidi ya asilimia 70 ya ukuaji wa uchumi ili kusaidia kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Dkt. Chaya pia alizitaja sekta za kilimo, madini, viwanda, nishati, huduma za kifedha pamoja na uchumi wa buluu kuwa na fursa kubwa kwa wawekezaji wa kimataifa huku akisema maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 yanafungua fursa mpya katika sekta za utalii, michezo, sanaa, burudani na miundombinu.
Zaidi ya makampuni 120 kutoka Urusi, makampuni zaidi ya 200 kutoka Tanzania pamoja na wajumbe zaidi ya 400 wameshiriki katika jukwaa hilo, hatua inayoonesha kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.










0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia